LIMEKUWA ni jambo la kawaida kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuandaa mipango mingi ya maendeleo kwenye makaratasi lakini utekelezaji haufanyiki ipasavyo.
Kabla ya kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/2017, shirikisho hili lilizitaka klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo kuwa na timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambazo zinatakiwa kucheza kabla ya timu za wakubwa.
Katika agizo hilo TFF ilidai kuwa timu yoyote ambayo haitakuwa na kikosi B itapokonywa pointi tatu kwa kushindwa kutekeleza agizo hilo, lakini utekelezaji haujafanyika na hakuna timu iliyopewa adhabu hiyo.
Kwa mfano, imekuwa kama desturi kwa timu za vijana za Simba na Yanga kukutana kabla ya zile za wakubwa kucheza, lakini baada ya hapo timu hizi za vijana hazijulikani zilipo.
Hivyo, kwa zoezi hili ni wazi TFF wamechemka kwani si kweli kwamba timu zinazoshiriki ligi kuu hazina vikosi vya vijana, bali linakwamishwa na mipango na mikakati mibovu ya TFF katika kuhakikisha linafanyika.
Lakini baadhi ya timu zinazoshiriki ligi kuu msimu huu zikiwemo Simba, Yanga na Azam zimejitahidi kutekeleza agizo hilo kwa michezo yao kutanguliwa na mechi za timu za vijana.
Idadi hiyo ni kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi msimu huu ambapo nyingine zilizobaki zimeshindwa kutekeleza kwa madai ya kukwamishwa na gharama za kusafirisha timu za vijana.
Kanuni hizo zimeandaliwa na kuwekwa na TFF kwa manufaa ya soka la Tanzania linalohitaji maendeleo hasa kwa kupitia vijana, hivyo ni wajibu kwa wanachama wake kulitekeleza.
Lakini jambo la kushangaza ni kwamba hakuna hatua zozote zinazochukuliwa na shirikisho hilo kutokana na baadhi ya wanachama wake ambao ni klabu kwa kushindwa kuonyesha ushirikiano.
Hali hii inaonyesha wazi kuwa TFF haina makali kwa wanachama wake ambao hawazingatii wala kuonyesha juhudi zitakazoleta faida kwa soka la Tanzania na badala yake wanatoa kipaumbele kwa mambo yanayorudisha nyuma mchezo wa soka.
Kama timu ina uwezo wa kuwaweka wachezaji kambini sehemu za gharama haiwezi kupata  tabu ya kuisafirisha timu ya vijana, hivyo huenda TFF imekubali kuburuzwa na wanachama wake.
Kama dhambi hii itaendelea kuitafuna TFF, ni wazi kwamba meno yake hayana makali kwa wale wanaowaongoza hivyo kuchangia kushuka kwa soka la vijana.