24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wodi za wagonjwa MOI zabatizwa jina la gereza

Almas Jumaa
Almas Jumaa

Na VERONICA ROMWALD–DAR ES SALAAM

BAADHI ya wagonjwa wameamua kuzipachika wodi mpya za Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) jina la gereza kutokana na kutopewa kabisa huduma au kupewa huduma zisizoridhisha.

Kitendo cha wagonjwa hao kutopewa kabisa huduma au kupewa huduma zisizoridhisha, kinadaiwa kusababisha mifupa yao iliyovunjika kujiunga yenyewe.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti juzi kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, wagonjwa hao waliolazwa wodi namba nne na namba tisa zilizopo katika jengo jipya la Moi, walisema wenzao wanaoteseka zaidi ni wale wasiokuwa na ndugu Dar es Salaam.

“Kimsingi hakuna yeyote ambaye anatamani kuugua na iwapo wanadamu tungepata nafasi ya kumwona Mungu basi wengi wetu ombi la kwanza lingekuwa ayaondoe kabisa maradhi.

“Lakini yapo na tunaumwa, sehemu pekee ya kwenda kupata huduma ya matibabu ya kisasa ni hospitalini kwa wataalamu bingwa na wabobezi wa masuala ya afya, lakini tunapokuja huku tunakutana na changamoto nyingi kiasi cha kutukatisha tamaa,” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano mimi nina mwezi sasa hapa wodini nilikuja kupata matibabu nimevunjika mguu nimetokea mkoani, katika kipindi hicho cha mwezi mmoja nimeshuhudia mengi humu ndani (jengo jipya), katika wodi niliyolazwa nimeshajionea wagonjwa watatu wakikata roho mbele yangu.

“Wagonjwa wale hawakuwa na ndugu hapa Dar es Salaam, walifika muda mrefu hapa hospitalini lakini hawakupata matibabu kwa sababu hawakuwa na fedha.”

Alisema ingawa kipo kitengo cha ustawi wa jamii ambacho wengi huenda kujieleza ili wasaidiwe, lakini huwa inachukua mchakato mrefu kwa sababu chenyewe huzidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa.

“Kwa hiyo mgonjwa unajikuta unaendelea kukaa wodini hadi maumivu yanakata na wapo ambao huamua kurejea nyumbani huku wakiwa hawajatibiwa kabisa, huwa najiuliza maswali mengi mno wanaenda kuishi namna gani maana wanapoondoka hapa hali zao huwa si nzuri, binafsi nashukuru angalau kitengo hicho cha ustawi wa jamii kinanisaidia na nimeambiwa si muda mrefu na mimi jina langu litawekwa kwenye orodha ya watakaofanyiwa upasuaji,” alisema.

Mgonjwa mwingine alisema wagonjwa wanaoteseka zaidi hospitalini hapo ni wale wasiokuwa na ndugu (waliotoka mikoani) na wale wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu.

“Kwa kuwa huna uwezo inabidi upitie njia ya ofisi ya ustawi wa jamii ili kupatiwa msamaha wa matibabu, hadi kufikia kufanyiwa upasuaji ndugu yangu, unakuwa umesota humu ndani hadi unakaribia kukata tamaa mwenyewe ndiyo maana mwenzangu anakuambia wengine huondoka wakiwa hawajatibiwa,” alisema.

Mgonjwa mwingine alisema yeye ni mmoja wa waathirika wa vitendo hivyo kwa sababu alijikuta akipangiwa kalenda kwa zaidi ya mara mbili.

“Yaani unapewa tarehe, ukija siku hiyo unaambiwa kalenda imejaa, unapangiwa tena tarehe nyingine, kwa kweli nilitaka kukata tamaa lakini nikajipa moyo na sasa nimeshafanyiwa upasuaji,” alisema.

Mgonjwa huyo aliendelea kusema kuwa kitendo cha kupangiwa tarehe na kuambiwa kalenda imejaa kinawafanya wagonjwa wengi wahisi pengine madaktari wa hospitali hiyo wanachukua rushwa kwa wale wanaofika na kupewa tarehe zao.

“Maana mambo haya tunakuwa tunayaona wazi, umepewa tarehe anakuja mwenzako na anapewa ile yako wewe unaambiwa siku hiyo imejaa, unakuwa huna jinsi zaidi ya kurejea nyumbani kwenda kuugulia maumivu,” alisema.

Mgonjwa mwingine alisema: “Ndiyo maana inafika wakati tunaona MOI ni sawa na gereza kwetu, hakuna anayependa kukaa hospitalini ndugu mwandishi, wote hapa maombi yetu kwa Mungu ili tupone tutoke wodini twende tukafanye kazi na kujenga uchumi wa nchi kama wengine, tunaomba Serikali itusaidie,” alisema.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MOI, Almas Jumaa, ambaye alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wagonjwa hulazimika kukaa muda mrefu kusubiri huduma ya upasuaji kutokana na sababu mbalimbali.

“Zipo sababu zinazosababisha kutokea kwa hali hiyo, kwa mfano ile ya upatikanaji wa vifaa tiba, kuna wakati unakuta vipo lakini mtu anakuwa anahitaji kifaa maalumu kulingana na maumbile yake.

“Hivyo hatuwezi kumwondoa wodini pasipo kumtibia inabidi tumlaze wodini asubiri kifaa hicho kinachotakiwa ili apate matibabu,” alisema Jumaa.

 

Pia alisema wakati mwingine mchakato wa kupata kifaa husika huchukua muda mrefu hasa wakati wa uagizwaji.

“Vifaa vyetu vingi tunanunua toka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pamoja na dawa, lakini kuna wakati tunalazimika kuagiza wenyewe toka nje ya nchi, hadi kifaa kifike hapa na kihakikiwe na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) huwa ni mchakato mrefu na inapotokea wanaishiwa wagonjwa hulazimika kukaa muda mrefu wodini kuvisubiri,” alisema.

Kuhusu suala la watumishi kupokea rushwa, Jumaa, alisema si kweli.

“Hakuna jambo hilo, ukweli ni kwamba MOI huwa tunapokea wagonjwa wengi wakiwamo wale wa dharura, sasa anapokuja mgonjwa wa dharura kwa mfano amepata ajali na anahitaji huduma ya haraka kuokoa maisha yake, watu wanaona ni rushwa.

“Ndipo pale madaktari wanapangua ratiba, kwa kuwaondoa wale wasiohitaji huduma ya dharura katika orodha na kuwahudumia wale wa dharura, pengine ndipo hisia za rushwa zinapotokea, nawahakikishia wagonjwa kwamba tupo kwa ajili ya kuwahudumia wote pasipo upendeleo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles