23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi wapekua nyumba ya Lema

lema-boy
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

 

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limefanya upekuzi wa zaidi ya saa moja katika nyumba anayoishi Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Nyumba hiyo iliyopo eneo la Njiro ilipekuliwa jana wakati Lema akiendelea kushikiliwa na polisi tangu Alhamisi wiki hii kwa mahojiano baada ya kukamatwa akiwa bungeni mjini Dodoma na kusafirishwa hadi mkoani hapa.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema hawezi kutoa taarifa za mambo ya upelelezi.

“Hayo ni mambo ya kiuchunguzi hatuwezi kutangaza taarifa leo (jana) tunamhoji au kupekua mtu nyumbani kwake hapana. Hatuwezi kutoa taarifa za kila kitu tunachofanya,” alisema Mkumbo.

Hata hivyo, mke wake mbunge huyo, Neema Lema, alisema ni kweli polisi wakiwa na magari manne, askari wenye silaha wakiongozana na OC CID Damass Massawe, walifika nyumbani kwake kupekua.

“Sikuwepo nyumbani kwa wakati huo. Nilikuwa nje kidogo ya mji eneo la Kisongo kumwona dada yangu wakati wao wakipekua. Lakini taarifa zote nimezipata kwamba wamepekua nyumba nzima kasoro chumba tunacholala kwa sababu nilikifunga na kuondoka na ufunguo,” alisema Neema na kuongeza:

“Kwa kweli hawakuondoka na kitu chochote. Lakini pia hawakusema wanatafuta nini na ili tu uone hakuna wanachokitafuta ni kwamba tangu juzi walipoanza kumshikilia hadi leo (jana) walikuwa hawajamhoji.”

Wiki iliyopita Lema akiwa bungeni mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge alikamatwa na polisi kisha akasafirishwa usiku hadi mkoani Arusha kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazodaiwa kumkabili.

Akithibitisha kushikiliwa na kuhojiwa kwa Lema, Mkumbo, alisema ni kweli alikuwa anaendelea kushikiliwa katika mahabusu iliyopo Kituo Kikuu cha Polisi.

“Ni kweli tunamshikilia yupo mahabusu, tunaendelea kumhoji kuna mambo bado tunakamilisha ya kiuchunguzi, tukimaliza kumhoji tutamfikisha mahakamani,” alisema Mkumbo.

Lema alikamatwa Novemba mosi, mwaka huu akidaiwa kutoa lugha zenye uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli katika mikutano yake ya hadhara jimboni kwake na alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana.

Akifafanua madai hayo, Mkumbo, alisema zipo baadhi ya tuhuma ambazo hawakumhoji na kukamatwa kwake ni mwendelezo wa upelelezi kabla hawajamfikisha mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles