KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameiomba Jamhuri ya watu wa China kurejesha upya utaratibu wa madaktari wa nchi hiyo wanaokuja kufanyakazi hapa kukaa miaka miwili badala ya mwaka mmoja wa sasa.
Mohamed ametoa kauli hiyo leo Mei 22, Mjini Unguja wakati alipokutana na ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka Mji wa Xuzhou ambao upo Zanzibar kufanya tathmini ya Madaktari wanaokuja kufanya kazi nchini katika hospitali ya Abdlah Mzee Mkoani Pemba na Mnazi mmoja Kisiwani Unguja.
Amesema tokea kuanzisha uhusiano wa madaktari wa China kuja Zanzibar mwaka 1965 walikuwa wakikaa kipindi cha miaka miwili lakini utaratibu huo ulibadilika miaka ya hivi karibuni na hivi sasa wanakaa mwaka mmoja.
“Madaktari wa Zanzibar wanapopata uzoefu kwa vitendo kutoka kwa madaktari wa China inawasaidia kufanya vizuri wanapopata nafasi ya masomo ya juu nje ya nchi” amesema.
Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo Zhou Guangchum amemuhakikishia Waziri wa Afya kwamba nchi yake itaendelea kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuongeza msaada wake hasa katika sekta ya afya.