Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima ameyataka Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali kushirikiana na Serikali kufikisha elimu ya chanjo ya Uviko 19 kwa wananchi huku akisisitiza chanjo hiyo ni ya hiari kama alivyosisitiza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Septemba 29,2021 Jijini Dodoma wakati akifungua semina elekezi kwa viongozi wa Mashirika Yasiyoyakiserikali (NG’Os),Waziri Gwajima amesema wanatambua kazi kubwa inayofanywa na mashirika hayo ambapo amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu juu ya chanjo ya Uviko 19.
Waziri Gwajima amesema suala la chanjo ni hiari na Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza katika mikutano yake hivyo Mashirika hayo yanawajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na jambo hilo.
“Napenda kusisitiza pia na kuwakumbusha kwamba chanjo hii ni hiari na Mheshimiwa Rais amekuwa akikumbusha kila mara anapokwenda kwenye mikutano yake na kuwakumbusha watanzania wajitokeze wakachanje kwa hiari.
“Nia yake Rais ni kuona Taifa lipo salama na Uviko 19 kwa kutekeleza afua za kinga ikiwemo afua ya chanjo kwa hiari dawa ya hiari ni elimu amesema Rais wetu elimu ya kutosha hili amelisisitiza.
Hivyo nitumie nafasi hii kuwakummbusha nyinyi kama wadau wenye majukumu mbalimbali na uelewa wenu mkubwa na uzoefu wenu mkashirikiane na wataalamu wetu wa afya na sekta zote mkasimamie na kuwezesha suala la elimu.
“Elimu itolewe kwa wananchi na suala la dhana ya uhiari likafanyike vizuri kwa kuwekeza kwenye msingi wa elimu kama alivyosema mheshimiwa Rais.
“Ikatokea mahala watu wengine wakataka kupotosha nia njema ambayo Rais amesema bahati nzuri wale watu wakaomba msamaha tulishasema ‘speech’ za viongozi ni suala nyeti kabla hujaamua kutoka nayo hakikisha umeilewa,”amesema.
Aidha,Waziri Gwajima amewashukuru wananchi kwa jinsi ambavyo wameipokea kampeni hiyo ambapo amedai Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
“Wizara itaendelea kushirikiana nanyi katika kutekeleza dhamira kubwa ya Rais ya elimu kukubaliana na Uviko 19.Mashirika yasiyokuwa yakiserikali mshirikiane na kule chini ili kila sikio likasikie ili kutekeleza afua hii,”amesema.