Na ATUPENDA GEOFREY (MPS)
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA zinazohusika na kutoa leseni za biashara za vileo nchini zimeshauriwa kudhibiti kushamiri kwa biashara hiyo, hususan jijini Dar es Salaam, ili kupunguza ongezeko la baa zilizochipua hadi kwenye makazi ya watu.
Wito huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Grace Shaba, ambaye ni katibu wa chama cha kisichokuwa cha kiserikali (NGO) cha Girl Guides Tanzania, ambaye alisema kwa sasa baa zimekuwa nyingi kiasi cha sehemu nyingine kuchukua nusu ya mtaa mzima.
Alisema kuwa licha ya kwamba kilevi hakiruhusiwi kuuzwa kwa vijana chini ya miaka 18, bado watoto wameendelea kushawishika na kujikuta wakitumia pombe.
“Kwa sasa unywaji wa pombe ni mkubwa sana jijini Dar es Salaam na cha ajabu ni kuwa leseni hizo zimekuwa zikitolewa hata kwenye maeneo ya makazi, jambo ambalo linadaiwa kusababisha mpaka watoto wadogo kujiingiza kwenye ulevi.
“Hivyo ni vyema Serikali ianze kuweka mkazo kwa kuhakikisha kuwa utoaji wa leseni unazingatia maeneo ya sehemu husika zinazouza vileo ili kupunguza janga hili kwa watoto,” alisema Grace.
Mdahalo huo ulihusisha wanafunzi ambao walikuwa wakishiriki katika mradi wa kuzuia vilevi mbalimbali kwa watoto ambao ulianza miaka mitatu iliyopita na unatarajiwa kumalizika mwaka huu kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Iringa.
“Mradi huu umeanzishwa kwa lengo la kuzuia matumizi ya vilevi mbalimbali, ambapo tumefanikiwa kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa kuhakikisha kuwa baadhi ya baa zilizokuwa zinafunguliwa kuanzia asubuhi hadi jioni hazifunguliwi tena.
“Lakini pia kwa wazazi ambao walikuwa na tabia ya kuwatuma vilevi watoto wao, tabia hiyo imepungua kufuatia wazazi wengi kubaini athari za tabia hiyo,” alisema Grace.
Ofisa Elimu Msingi Vifaa na Takwimu Manispaa ya Kinondoni, Marietha Kayombo, alisema pombe ni adui wa haki na kwamba haina budi kuhakikisha kuwa inakomeshwa kuuzwa kwa wanafunzi.
“Mradi huu umesaidia kwa kiwango kikubwa katika Manispaa yangu ya Kinondoni ambapo umesaidia shule nyingi watoto kupata ufahamu juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya vilevi.
“Hivyo wazazi hawana budi kuhakikisha wanawakagua watoto wao kwa kujua mienendo yao, njia wanazopita kwenda shule, lakini pia kujenga urafiki na walimu ili kuhakikisha kuwa wanatambua tabia za watoto wao kuliko tu kuishia kukagua madaftari yao,” alisema Marietha.
Mwisho ……….