27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Witness: Namtamani zaidi Basta Ryhmes

WITNESS9NA GLORY MLAY

KATI ya wanadada wanaofanya vizuri katika muziki wa kurap nchini ni Witness Mwaijaga ‘Kibonge Mwepesi’.

Mwanadada huyu licha ya kujua kucheza na maneno katika rap zake, pia ana uwezo wa kuimba na kunengua licha ya kuwa na mwili mkubwa usiodhaniwa kufanya anachoweza kufanya.

Mwanadada huyo ambaye ni mpenzi wa msanii mwenzake wa Bongo Fleva, Ochu Sheggy, anayetamba na wimbo wa ‘Shemeji yako’, anasema wasanii wengi wa kike wanapotea katika muziki kwa kuwa asilimia kubwa ya maisha yao wamewekeza katika masuala ya ndoa.

Witness aliyewahi kuwa katika kundi moja la muziki na marehemu Langa na mkali mwingine anayetamba na wimbo wa ‘Sugua Gaga’, Shaa anasema kwa sasa mawazo yake bado hayafikirii kuolewa kwa kuwa anataka awekeze zaidi katika muziki wake.

“Sijafikiria kuwekeza maisha yangu katika ndoa kwa kuwa nitakosa uhuru wa kufanya mambo yangu, inabidi niachane na muziki nihudumie familia, wanaume wengi hawataki uendelee na muziki akishakuoa jambo ambalo silipendi.

“Msichana lazima uolewe lakini tunatakiwa tuwekeze kote kwenye ndoa na muziki na kama inashindikana tuwekeze zaidi katika muziki baada ya kufanikiwa kimuziki ndiyo tuwekeze katika ndoa kwa kuwa tutaweza kuendelea na muziki lakini kama hakuna mafanikio ni rahisi kuachana na muziki baada ya ndoa.

Witness anasema muziki wa zamani ulikuwa unaeleza zaidi hisia na matukio ya kweli wasanii wa zamani walikuwa wanawekeza katika muziki kikweli kweli tofauti na sasa wasanii wanaangalia namna gani watapata fedha hata kama muziki wao si mzuri na haufai kwa jamii.

Witness anaongeza kwamba kutokana na wasanii kutojitambua na kutowekeza kikamilifu katika muziki wao wengi wao wameingia katika utumiaji na hata uuzaji wa dawa za kulevya.

“Ni shida sana kumshauri mtumiaji wa dawa za kulevya hasa msanii maana wengi wao hutupuuza tunapowashauri lakini huja kujutia baada ya kugundulika na wengi hakuna ushujaa wa kutumia dawa za kulevya wanatakiwa waache hakuna faida kwao zaidi ya aibu na kuipa mzigo mkubwa familia na marafiki zako,’’ anaeleza.

Katika hatua nyingine, Witness anasema msanii anayependa kazi zake na muziki wake kwa Tanzania ni mchumba wake, Ochu Shagy, kutokana na kuwa na muziki tofauti na wasanii wengine ndiyo maana alivutiwa naye hadi kimapenzi.

“Kwa nje namtamani zaidi Basta Ryhmes kwa sababu naona tunaendana kimuziki, tukifanya kolabo itakuwa nzuri sana maana anafanya ninachofanya kwa hapa Bongo ila sipendi kolabo kwa kuwa inaonyesha kama unalazimisha kuwa juu kupitia unayeshirikiana naye,” anamaliza Witness ambaye starehe yake kubwa ni kuogelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles