23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Coastal kuchuana Kombe la FA leo

smbNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Simba leo itashuka dimbani kuvaana na Coastal Union katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la FA utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba watashuka dimbani kuikabili Coastal huku wakiwa na rekodi nzuri ya kutoa vipigo mara mbili msimu huu kwa timu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ni ushindi wa bao 1-0 katika mzunguko wa kwanza na 2-0 waliporudiana Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Wekundu hao wa Msimbazi wataingia uwanjani kusaka ushindi wa pointi tatu muhimu mbele ya ‘Wagosi wa Kaya’ ili waweze kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na kuzifuata timu za Yanga, Azam na Mwadui FC ambazo tayari zimefuzu hatua hiyo.

Mahasimu wao Yanga waliingia nusu fainali baada ya kuichapa Ndanda FC mabao 2-1, Azam ilifanikiwa kwa kutoa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons, huku Mwadui ikiwafunga Geita Gold Sport mabao 3-1.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo kocha wa Simba, Jackson Mayanja, alisema kikosi chake kipo kamili kuwavaa wapinzani wao hasa baada ya kurejea kwa mshambuliaji, Hamis Kiiza na beki, Jjuuko Murshid na kujiunga na wenzao mazoezini.

Alisema wachezaji hao wamechelewa kujiunga katika mazoezi ya pamoja kujiandaa na mchezo huo, lakini anaamini timu yake itafanya vizuri na kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la FA kulingana na programu na mbinu alizofundisha.

Kiiza na Jjuuko walishindwa kurejea nchini kwa wakati baada ya kumaliza majukumu ya kuichezea timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Burkina Faso.

Katika hatua nyingine, kocha huyo raia wa Uganda alisema hana uhakika wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwa kuwa nafasi bado ipo wazi kwa timu zote zinazoshika nafasi tatu za juu.

Alisema hali hiyo inasababishwa na ushindani wa mbio za ubingwa uliopo Ligi Kuu, huku akidai kiufundi ni vigumu kufanya utabiri kwa Simba pekee kwa kulinganisha na mechi zilizobaki wakati wapinzani wao Yanga na Azam bado wana mechi za viporo.

“Nitaendelea kusema kwamba bado mambo ni magumu, hadi ligi itakapomalizika ndio kitaeleweka, kwa sasa kila timu hasa zinazoshika nafasi tatu za juu ndiyo zipo katika nafasi ya kunyakua ubingwa msimu huu,” alisema Mayanja.

Simba ndio wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 57 baada ya kushuka dimbani mara 24, wakifuatiwa na Yanga waliojikusanyia pointi 53 kwa kucheza michezo 22, huku Azam wakishika nafasi ya tatu kutokana na pointi 52 walizovuna katika michezo 23 waliyocheza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles