TANGU Serikali ya awamu ya tano iingine madarakani, tumeshuhudia hatua mbalimbali zikichukuliwa kwa watendaji wa Serikali ambao kwa namna moja au nyingine hawaendani na kasi inayotakiwa.
Gatua hiyo ilipewa jina la tumbua tumbua ambalo kwa kweli kila mmoja wetu ameshuhudia viongozi wakubwa wakitumbuliwa kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kufanya maboresho.
Inawezekana kabisa kwamba tumbua tumbua hii, ina lengo la kujenga upya sehemu ambazo zinaonekana wazi ama zimepwaya au hazifiki malengo yaliyokusudiwa na mamlaka za juu.
Lakini si nia yetu kueleza mlolongo mzima wa utumbuaji huu. Leo tumelazimika kuandika tena juu ya jambo hili baada ya kushuhudia kila baada ya siku kadhaa, utasikia bodi fulani imevunjwa kwa kile kinachodaiwa haitimizi majukumu yake.
Hatupingi hata kidogo uamuzi unaochukuliwa kila wakati, bali tunajiuliza hiyo kazi ya kuvunja bodi kila kukicha inaleta manufaa au mabadiliko makubwa kwa mara moja? Jibu ni kwamba lazima ijipe muda.
Wiki iliyopita Rais John Magufuli alivunja Bodi ya Korosho Tanzania kutokana na matatizo yaliyojitokeza juu ya zao la korosho kukosa soko la uhakika.
Tumeshuhudia jana, Rais Magufuki amechukua uamuzi mgumu wa kulituma Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi kuanza kazi ya kusomba korosho na kuzipeleka Dar es Salaam.
Tunasema uamuzi ni mzuri, lakini tunarejea kwenye msingi wa uvunjaji wa bodi hizo ambazo zipo na zimekaa  madarakani kwa mwaka mmoja au mmoja na nusu, lakini kukaibuka matatizo.
Hali hiyo imeendelea jana mkoani Dodoma, baada ya Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani naye kutangaza kuivunja bodi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa  Umeme Vijijini (REA) kwa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti, Gideon Kaunda na wajumbe wake.
Akitangaza uamuzi huo, Waziri Kalemani alisema uamuzi huo umetokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wa bodi hiyo kwa kipindi chote ambacho imekuwa madarakani.
Tunatambua wazi kwamba waziri anayo mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa kifungu 9(3)(b) cha Sheria na.8 ya Nishati Vijijini ya 2005 kuvunja na kuisuka upya bodi iliyo chini yake, lakini tunashtushwa na wimbi hili ambalo limechukua kasi katika siku za karibuni.
Bodi hiyo ambayo iliundwa mwaka jana, imetekeleza majukumu yake kwa takribani mwaka mmoja sasa, muda ambao kwa kweli ni mfupi mno.
Tunajiuliza maswali mengi, inakuwaje bodi inavunjwa ndani ya mwaka mmoja wakati waziri na timu yake nzima wapo. Hivi huwa hawaoni mwenendo wa utendaji kazi wake?
Tunaamini siku zote za utendaji kazi wa bodi kuna vikao vya msingi ambavyo waziri, naibu wake na katibu mkuu huwa wanahudhuria na kupata mrejesho wa kila kitu kinachofanyika au kinachotarajia kufanyika.
Tunasema hivyo kwa sababu desturi hiyo ikiendelea, watendaji wengi katika bodi hizo watashindwa kupanga mipango yao ya kuendesha mashirika au makampuni makubwa kwa kujawa na hofu ya kutumbuliwa wakati wowote. Jambo hilo linapaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu kwa manufaa ya taifa.
Hatupingani na mamlaka zinazohusika, bali tunashauri hata wakataoteuliwa kushika nyadhifa hizo hasa katika eneo kama REA, basi watambua namna ambavyo Watanzania wengi wana mahitaji muhimu ya kupata nishati hiyo.
Tunasisitiza hilo kwa sababu uamuzi wowote ambao unafikiwa na bodi ndiyo uti wa mgongo wa kutatua matatizo yanayowasibu Watanzania kwenye maeneo husika.Ndiyo maana tunasema uvunjaji huu wa bodi uangaliwe vizuri.