Na RATIFA BARANYIKWA-DAR ES SALAAM Â
HII ni wiki ya tatu tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iruhusu kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuanza, tofauti na wiki ya kwanza na ya pili hii inaonekana kuwa na taswira nyingine.
Taswira yenyewe ni kwamba wagombea wawili kutoka vyama viwili kwa upande wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na visiwani Zanzibar ndio wanaoonekana kuteka majukwaa ya kampeni ama kwa lugha ambayo tumeizoea mtaani ‘wana-trend’.
Watu wanaofuatilia mwenendo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2020 watakubaliana na mimi kwamba kwa upande wa wagombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ‘wanao-trend’ ni hawa watu wawili; Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tundu Lissu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kwa upande wa urais wa Zanzibar ‘wanao-trend’ ni wawili tu, Dk. Hussein Mwinyi wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama za ACT -Wazalendo.
Wiki hii ya tatu tangu kampeni kuanza kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano na wiki ya kwanza kwa upande wa Zanzibar, mambo mawili yamebadilisha upepo wa wiki mbili zilizopita.
Jambo la kwanza, ni hili la mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Bernard Membe ambaye alionekana pengine angeweza kuleta ushindani mkubwa, sasa pumzi ni kama inaonekana kukata katika wiki hii ya tatu.
Ingawa ni mapema kuhitimisha hilo, haijulikani kama Membe anaweza kufanya maajabu katika wiki zilizobaki hasa ikizingatiwa kwamba katika wiki hii ya tatu baadhi ya mitandao ilimwonyesha akikwea ndege kuelekea nje ya nchi.
Hilo linathibitishwa aliporejea mapema wiki hii, ambapo mara baada ya kutua Dar es Salaam, alisikika akidai kuwa msaidizi wake ametekwa na watu wasiojulikana.
Madai yaliyojibiwa mara moja na Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyesema msaidizi huyo wa Membe, Jerome Luanda alikuwa mikononi mwao akihojiwa kuhusu tuhuma za utakatishaji wa fedha.
Jerome Luanda alikamatwa baada ya kurejea nchini akitokea Dubai katika Muungano wa nchi za kiarabu ambako aliambatana na Membe.
Membe awali alitangaza kuwa anakwenda Dubai kwa matibabu.
Pamoja na hayo dalili za kasi ya Membe kwenye kampeni kupungua zilianza kuonekana wiki ya pili kiasi cha kuzua minong’ono kwamba chama chake kilikuwa kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.
Hata hatua yake ya kwenda Dubai ambako yeye mwenyewe alisema amekwenda kwa matibabu kulijenga picha kwamba huenda amekwenda kutafuta njia ya kupata fedha za kuendeshea kampeni.
Minong’ono hiyo haijawahi kuthibitishwa na Membe wala chama chake, hivyo inabaki kama taarifa za kimbea za makoridoni.
Kutokuwepo Membe katika wiki hii ya tatu hali kadhalika pamoja na dalili zile za mwanzo za kusuasua kwa kampeni zake, kumetoa uwanja kwa wagombea wawili wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Magufuli na Lissu kuonekana kuwa wao ndio wanaochuana kwa ukaribu na walioteka kampeni hizi.
UPEPO MWINGINE
Jambo la pili lililojitokeza katika wiki hii ya tatu, ni mgombea huyo wa upinzani, Lissu mikutano yake kuoneknaa kuongezeka na kuzidi kuvuta watu kila kukicha si tu yeye bali na wagombea wa nafasi nyingine za ubunge na udiwani wa chama chake.
Hali hiyo imekuwa tofauti na matarajio yangu binafsi pamoja na ya watu wengine wengi si ajabu hata ndani ya CCM.
Kutokana na misukosuko dhidi ya upinzani, staili ya uongozi wa miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya tano, ambayo ilionekana wazi kuzima kelele za vyama vya upinzani kuanzia mitaani hadi bungeni hali kadhalika kwenye baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo, wengi wetu hatuamini kile tunachokiona sasa kwenye mikutano ya vyama hivi vya upinzani hususani Chadema, ambavyo tulijua vimekwisha.
Chadema sasa wanaonekana kuwanyima usingizi wagombea wa CCM wa nafasi mbalimbali tofauti na mawazo ya mwanzoni.
Chadema na CCM ni miongoni mwa vyama 15 vinavyoshiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Vyama vingine ni pamoja CUF ambacho nafasi yake ni kama sasa inaonekana kuchukuliwa na ACT-Wazalendo ‘inayo-trend’ mbele yake.
Vyama vingine vinavyoshiriki ni, Chaumma, UPDP, SAU, NCCR- Mageuzi, DP, AAFP, ADC, NRA, NLD na ADA-Tadea ambavyo licha ya baadhi kuzindua kampeni havijasikika tena.
ZANZIBAR
Kwa upande wa Zanzibar ambako hii ni wiki ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa kampeni zake kama nilivyosema hapo juu, nako wagombea wanaochuana vikali ni wawili tu, Maalim Seif na Dk. Mwinyi.
Mwinyi anachuana safari hii ni Chama cha ACT-Wazalendo chini ya Maalim Seif ambacho miaka mitano iliyopita hakikuwa kwenye orodha ya vyama vitatu vilivyokuwa juu.
Katika kampeni za sasa chama hiki kinaonekana kuchukua nafasi ya Chama Cha Wananchi, CUF kilichokuwa na mizizi mikubwa Zanzibar.
CUF bado kinachojikongoja kutoka kwenye vidonda vya migogoro wa tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Katika chaguzi takribani zote chini ya mfumo wa vyama vingi, kwa mara ya kwanza CUF inaonekana kukaa nje ya mchuano mkali kwa sababu ya vidonda vya mgogoro wa kiuongozi.
Chama cha ACT-Wazalendo kimekalia nafasi ya CUF, chama hicho hata katika chambuzi zangu huko nyuma niliwahi kusema kinawaacha wengi katika maswali na mjadala wa jinsi kilivyoanzishwa na kukua kwa kasi huku waasisi wake karibu wote wakiwa wametimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwamo mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Anna Mghwira ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Jabali la siasa za upinzani Visiwani Zanzibar aliyekibeba CUF kwa takribani miaka 29 zaidi kwa mbeleko imara na hata kufanikiwa kukitikisa CCM kwa miaka yote, Maalim Seif Sharif Hamad ndiye aliyeiongezea umaarufu ACT – Wazalendo yeye na wenzake wanaonekana kukipa nguvu chama hicho katika kampeni hizi dhidi ya CCM ya Dk. Mwinyi.
Maalim Seif yupo ACT-Wazalendo baada ya mgogoro mkubwa wa kikatiba na kiuongozi na Mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba, uhasama ambao tangu mwanzo hata kabla ya kuanza kwa kampeni ulionekana wazi kukidhoofisha CUF na hivyo kwa mara ya kwanza kujikuta kikitoka kwenye mstari wake.
Maalim Seif na timu yake iliyokuwa ikitikisa siasa za Zanzibar safari hii wameajipanga katika mazingira tofauti ya ACT- Wazalendo, chama ambacho hata katika uchaguzi wa mwaka 2015 hakikuwemo kwenye ushirika wa vyama vya upinzani ambao ulitikisa kura za urais wa Dk. Shein na nafasi nyingine visiwani humo.
Chama hicho katika uchaguzi wa 2015 kiliambulia mbunge mmoja tu.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wakati ACT-Wazalendo ikijiweka kando, vyama vinane viliungana chini ya ubatizo wa Ukawa na kumsimamisha mgombea wa urais, Edward Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97 huku Magufuli wa CCM akipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47.
Mbali na nafasi ya urais, vyama hivyo viliachiana majimbo kulingana na mgombea ambaye alikuwa akikubalika zaidi katika eneo husika.
Uchaguzi huo wa mwaka 2015 uliohusisha majimbo 258 kati ya 264, CCM ilishinda ubunge katika majimbo 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti kimoja. NLD haikupata kiti wakati ACT – Wazalendo ilipata kiti kimoja kilichochukuliwa na Zitto Kabwe kupitia jimbo la Kigoma Mjini.
Kwa hesabu hiyo, Chadema ilifikisha wabunge 70 kutoka 48 wa mwaka 2010, CUF ilipata wabunge 45 kutoka 36 wa mwaka 2010 wakati NCCR-Mageuzi ikishuka kutoka wabunge wanne wa 2010 hadi mmoja na kufanya idadi ya wabunge wa Ukawa kuwa jumla 116 na CCM ikifikisha wabunge 252.
Idadi hiyo ya wabunge wa upinzani ndiyo kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na baadaye kufanyika uchaguzi wa kwanza wa ushindani mwaka 1995.
Muungano huo wa vyama vya upinzani mwaka 2015 ambao ulibebwa na nguvu Muungano huo na vigogo wa siasa za upinzani hasa kwa upande wa visiwani Zanzibar, Maalim Seif na timu yake, kama akina Babu Duni Haji, Ismail Jussa na wengine visiwani humo ulikuwa ni wa vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.
Ukiacha CUF, vyama vingine vilivyokuwa vimeingia katika muungano huo havikuwahi kuwa na nguvu ya kufurukuta visiwani humo kama ilivyo kuwa kwa CUF ya Maalim Seif.
Kilichotokea mwaka 2015 na hata Tume ya Uchaguzi (ZEC) iliyokuwa chini ya Jecha Salum Jecha kulazimika ama kupenda au kutopenda kuitisha uchaguzi wa marudio, ni nguvu ya CUF iliyokuwa ikibebwa na Maalim Seif na timu yake ambayo sasa ipo ACT-Wazalendo.
Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na mwanasiasa kijana machachari, Zitto Kabwe ni cha tatu kwa Maalim Seif kujiunga nacho tangu alipoingia kwenye siasa.
Wakati mwelekeo wa kampeni za CUF ukionekana kupwaya katika wiki ya kwanza, wengi wanasubiri kuona kama katika siku zilizobaki kama kitaweza kufanya maajabu.
SI SIASA ZA MAJARIBIO
Dk. Mwinyi daktari kwa taaluma ambaye ametumikia serikalini kwa muda mrefu akiwa kama naibu waziri na baadae waziri kamili wa afya kabla ya kupewa Wizara ya Ulinzi katika serikali za awamu ya tatu, nne na tano akionekana kubebwa na haiba ya ustaarabu, kutopenda makuu kikwazo kikubwa kwake kuanzia kwenye majukwaa ni Maalim Seif ambaye kumshinda kwa hoja kwa mtu ambaye si mzungumzaji kunahitaji nguvu ya ziada.
Mwinyi, kama ilivyo kwa Rais anayemaliza muda wake, Dk Shein, Aman Karume na wengine naye anapita njia ile ile ya kupambana na Maalim Seif ambaye anawania nafasi hiyo kwa mara ya sita.
Mwinyi anapambana na Maalim Seif ambaye si tu anajua mapambano ya upinzani bali mtu anayeijua vizuri CCM kwani aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho kabla kutimuliwa mwaka 1988 akiwa na wenzake, Ali Haji Pandu, Soud Yusuf Mgeni, Shaban Mloo, Khatib Hasan, Hamad Rashid na Ali Salim.
Rekodi ya Maalim Seif binafsi na ile ya ndani ya CCM ni ndefu na isiyopaswa kupuuzwa kwani amewahi kuwa Mjumbe Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Elimu wa visiwa hivyo kati ya mwaka 1977-1980.
Pia amewahi kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la kati ya mwaka 1980-1989, Mbunge wa Jamhuri ya Tanzania mwaka 1977.
Aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kati ya mwaka 1977 hadi 1987 pamoja na kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango wa CCM.
Baadaye alikuwa waziri kiongozi wa Zanzibar kuanzia Februari 6, 1984 hadi Januari 22, 1988.
Pamoja na kutumikia nyadhifa hizo zote, Maalim Seif mwenyewe ambaye miaka ya hivi karibuni bila kutaja sababu alisema aliingizwa kwenye siasa ingawa haikuwa mipango yake, mwaka 1988 alitimuliwa CCM, kutokana na mgogoro wake na maofisa wa chama hicho.
Zipo taarifa zinazodai kwamba Maalim Seif alitimuliwa baada ya mgongano mkubwa wa maslahi ndani ya CCM Zanzibar, kati yake na aliyekuwa Rais wa visiwa hivyo Aboud Jumbe.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa chokochoko ya vigogo hao wawili ilitokana na Maalim Seif kumdokeza Mwalimu Julius Nyerere kuhusu azma ya Rais Jumbe kuhoji muundo wa muungano.
Jambo hilo linatajwa kumkasirisha Jumbe ambaye alichukua uamuzi wa kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damiani Lubuva na badala yake akataka kumwajiri mwanasheria kutoka Ghana.
Tangu kuondolewa kwake CCM, Maalim Seif si kuyumba, hajawahi kuchuja kisiasa na amekuwa akitikisa siasa za visiwa hivyo tangu wakati huo.
Katika miaka yote zaidi ya 30 Maalim Seif amepambana na CCM bila kuchoka, na bila kusalimisha silaha chini na kubwa alilolifanikisha ni kuundwa kwa nafasi ya makamu wawili wa rais wa Zanzibar.
Uvumilivu wa Maalim Seif ulionekana hata alipopita katika wakati mgumu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulipozuka mgogoro wake na Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliamua kuachia ngazi ya uenyekiti kwa hoja ya kutokubaliana na njia waliyotumia akina Maalim Seif na wenzao wa Chadema kupambana kusaka dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ambao vyama vya upinzani kikiwamo CUF kiliamua kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliyehama CCM kutokana na jina lake kukatwa kimizengwe.
Hata Profesa Lipumba alipoamua kurudi baada ya Uchaguzi Mkuu uliomwingiza madarakani Rais John Magufuli huku upande wa Zanzibar wakiamua kurudia uchaguzi uliomrudisha Shein, Maalim Seif aliposhindwa kutatua tatizo lake na Profesa Lipumba hadi kwenye vyombo vya sheria aliamua kumwachia chama alichoshiriki kukiasisi.
Kutokana na hayo, Mwinyi si tu anapambana na mtu mwenye misimamo bali anaingia kwenye orodha ya vigogo wakubwa ambao wamepambana na Maalim Seif katika chaguzi zote tangu mwaka 1995 kama akina Salmin Amour, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume ambaye ni Amani Karume mwaka 2000 na 2005 na mwaka 2010 na 2015 Dk. Shein.
Pia Mwinyi anapambana na Maalim Seif ambaye ni tofauti na wanasiasa wengine ambao wamekuwa wakiyumba yumba kama Augustine Mrema, mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na wanasiasa wengine, kwani tangu alipoondoka CCM hajawahi kurudi nyuma wala kuchuja licha ya umri wake tangu mwaka 2015 kuonekana kusogea.
HOJA ZA WIKI YA TATU
Kama ilivyokuwa wiki mbili zilizopita agenda ni mbili kubwa ambazo zinazoonekana kubebwa na wagombea wote katika kipindi chote hiki.
Agenda hizo ni maendeleo pamoja na haki na uhuru. Magufuli, Lissu, Dk.Mwinyi, Maalim Seif wote wanazungumza hayo hayo.
CCM kinazungumza matumaini ya maendeleo ambayo yamefanywa na serikali ya awamu ya tano na ya nane kwa upande wa Zanzibar kuwa ndiyo yanayoweza kuwabeba katika Uchaguzi Mkuu huu.
Hoja kubwa ambazo mgombea wa CCM ameendelea kuzibeba ni jinsi alivyoleta maendeleo pamoja na kuanisha mipango ya miaka mingine mitano.
Mgombea anayeonekana kuchuana naye kwa ukaribu kwenye kampeni, Tundu Lissu wa Chadema naye ameendeleza hoja zake zile zile maendeleo yenye sura ya haki lakini pia uhuru na haki.
Anasema maendeleo kama, ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa la umeme Rufiji, upanuzi wa barabara ni lazima yote hayo yaendane na haki ya kulipa fidia wananchi waliobomolewa kupisha upanuzi wa barabara, kutoa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wote wa umma na kutoa huduma kwa jamii bila kuikandamiza, wala kuionea.
Mwinyi na Maalim Seif wanahubiri Zanzibar mpya, mageuzi na mabadiliko makubwa ya kiuchumi visiwani humo.
Mwinyi ambaye wakati akizindua kampeni alionekana kubeba zaidi hoja ya uchumi wa bluu kwa maana ya kutumia bahari kufanya mapinduzi ya kiuchumi, Maalim Seif nae ana ndoto ya Zanzibar mpya.