25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

WhatsApp, Yahoo zatiliwa shaka kuhusu usiri wa data za watumiaji

Miongoni mwa mataifa yanayotuhumiwa kupora data za watumiaji ni Marekani
Miongoni mwa mataifa yanayotuhumiwa kupora data za watumiaji ni Marekani

CHOMBO kinachoratibu data cha Umoja wa Ulaya kimezitwanga barua kampuni za WhatsApp na Yahoo kuzitaka zijieleze kuhusu wasiwasi wa usiri wa data za watumiaji.

Kampuni ya Whatsapp, maarufu kwa huduma za ujumbe wa meneno imehojiwa kuhusu kubadilishana kwake taarifa na kampuni mama ya Facebook.

Na wakati huo huo, Yahoo imewekewa kibano kuhusu ukiukaji wa takwimu wa mwaka 2014 na kitendo cha ku-scan barua pepe za wateja wake kwa malengo ya kiintelijensia ya Marekani kwa mujibu wa ripoti.

Mamlaka ya kulinda data ya Umoja wa Ulaya (EU) ilieleza wasiwasi wake kuhusu mabadiliko yaliyofanywa na WhatsApp hivi karibuni kuhusu sera ya usiri ambayo itawafanya watumiaji wa simu kuchangia namba za simu na mtandao wa Facebook.

Haya yalikuwa mabadiliko ya kwanza ya kisera tangu Facebook ilipoinunua kampuni hiyo ya huduma za ujumbe wa maneno miaka miwili iliyopita.

Hatua hiyo yenye utata iliyoelezwa kistadi lakini iliyoashiria hatua muhimu kwa WhatsApp, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijitanabaisha kama kampuni inayojali na kulinda usiri wa watumiaji wake bilioni moja duniani.

WhatsApp imeshaanza kuratibu akaunti na Facebook kwa kuchangia namba za watumiaji wa simu za mikononi.

Pia hubadilishana taarifa kutika simu kama vile aina ya mfumo endeshi (operating system (OS)) na program nyingine za simu za kisasa.

Watumiaji wa Facebook hutumia namba za simu za watumiaji wa WhatsApp walio Facebook.

Hutumika pia kuvutia matangazo yanayoonekana na watumiaji wa mtandao wa facebook na kugawana mbali ya namba za simu pia na maelezo ya mara ya mwisho ya mteja kuingia katika akaunti yake ya WhatsApp na facebook.

Mamlaka, chini ya Ibara ya 29 ya Kazi, inaiamuru WhatsApp kuwasilisha taarifa zote muhimu kwa mamlaka kwa kadiri ya haraka iwezekanavyo na kusitisha kuchangia data za watumiaji hadi hatua za makusudi za kisheria za usiri zitakapohakikishwa, sehemu ya barua hiyo ya wiki iliyopita ilisomeka.

Ilipoulizwa kuhusu suala hilo, msemaji wa WhatsApp alisema kampuni hiyo ilikuwa ikifanya kazi na mamlaka za kulinda data na kushughulikia wasiwasi uliowasilishwa.

“Tuna mazungumzo ya kutia moyo ikiwamo na dhamira ya kuheshimu sheria zilizopo,’ alisema.

Katika ripoti iliyochapishwa wiki mbili zilizopita, WhatsApp na Facebook zilijigamba kwamba zi program salama zaidi kuzitumia, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Amnesty International.

Hata hivyo, wataalamu wa usalama wanapinga kuwapo kwa usalama huo unaodaiwa na kampuni hizo, wakisema zingeweza kufanya zaidi ya hatua waliyofikia ili kulinda data za watumiaji.

Ripoti ya Amnesty iliorodhesha kampuni11 ambazo zinaendesha program maarufu za ujumbe wa maneno ikiwamo Skype, Snapchat na Facebook Messenger.

Shirika hilo la haki za binadamu liliangalia namna kampuni hizo zinavyolinda usiri wa wateja na uhuru wao wa kutoa maoni.

Taasisi hiyo iliomba taarifa kutoka katika kampuni 11 za teknolojia, ambapo tatu BlackBerry, Google na Tencent – hazikujibu.

Shirika hilo liliandikia pia Yahoo kutaka ieleze ukiukaji mkubwa wa data zilizovujisha barua pepe milioni 500 za watumiaji pamoja na kuscan barua pepe za wateja ambazo zilikabidhiwa kwa maofisa wa usalama wa Marekani.

Wadukuzi wa mitandaoni wanaaminika kupora majina, anuani za barua pepe, namba za simu, siku za kuzaliwa, namba za siri na maswali ya usalama pamoja na majibu ya watumiaji wake milioni 500.

Mamlaka ziliitaka kampuni kuwasilisha maudhui yote ya ukiukaji wa data kwa mamlaka za EU, kuieleza watumiahji walioathirika na kushirikiana na mamlaka zote za uchunguzi.

Kesi za Yahoo na WhatsApp zinajadiliwa na wasimamizi wa mawasiliano mwezi huu.

Kiwango hicho cha wizi ni kikubwa mno katika historia ya udukuzi wa mitandaoni na Yahoo ilikiri hilo kutokea 2014 na kwamba ilikuwa haina habari wakati zikiibwa.

Wakosoaji walimtaka bosi wake, Marissa Mayer ajiuzulu baada ya kubainika mwezi uliopita kuwa aliwahi onywa juu ya uwapo wa njama za kudukua takwimu miezi miwili kabla.

Wadukuzi wanaoiba takwimu huzitumia kwa malengo mbalimbali ikiwamo kutishia watumiaji wa yahoo kumwaga siri zao iwapo hawatawapa fedha, kubomoana kisiasa au kibiashara na kadhalika.

Wakati ikijitetea Yahoo ilidai barua pepe hizo milioni 500 na maelezo ya kibenki yako salama na kwamba udukuzi ulifadhiliwa na serikali fulani, lakini ilikataa kuitaja nchi hiyo.

Taarifa hizo zimekuja huku wabunge nchini Marekani wakieleza wasiwasi wa usalama wa data za raia wa Marekani siku za usoni.

Hiyo inatokana na wimbi la kudukuliwa kwa taarifa za wanasiasa akiwamo mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton kunakodaiwa kuwa na mikono ya Urusi.

Aidha uamuzi wa sasa Ulaya unakuja pia baada ya Tume ya Mawasiliano nchini Uingereza kuanza kuchunguza uamuzi wa WhatsApp  kugawana data facebook.

Tume hiyo ilisema mabadiliko hayo yataathiri watu wengi na hivyo kutaka maelezo zaidi kuhusu kile kitakachogawanywa kati ya huduma hizo mbili.

Aidha facebook ilijikuta katika kibano cha sheria nchini Ujerumani baada ya kupigwa marufuku kuchukua data za watumiaji wa Whatsapp nchini humo.

Baada ya WhatsApp kukamilisha mikataba ya utumiaji kwa watumiaji wa app hiyo maarufu duniani, watu na mashirika mbalimbali yanayolinda haki za usalama wa data za watumiaji wa huduma za kimitandao walilalamika.

Mabadiliko hayo yaliyoletwa na app hiyo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na huduma hiyo kumilikiwa na Facebook ambayo ililipa dola bilioni 19 kuinunua mwaka 2014.

Facebook inayomilikiwa na Mark Zuckerberg iliona kwamba njia pekee ya kurudisha fedha hizo ni kuunganisha huduma ili waweze kunufaika kibiashara kutoka kwenye data zinazohusu mamilioni ya watumiaji wa WhatsApp duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles