24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

‘Serikali ianzishe programu kuwatambua walemavu wa akili’

Mshauri wa Kituo cha Kulea Watoto Walemavu kilicho chini ya Mfuko wa Kumbukumbu wa Eric, Josephine Bakita, akiwa na mtoto mwenye ulemavu
Mshauri wa Kituo cha Kulea Watoto Walemavu kilicho chini ya Mfuko wa Kumbukumbu wa Eric, Josephine
Bakita, akiwa na mtoto mwenye ulemavu

Na Lilian Justice, Morogoro

MTU yeyote mwenye ulemavu anapaswa kupewa haki sawa, kutambulika makazi yake, kupewa huduma za elimu, afya na malezi bila kujali aina ya ulemavu alionao.

Pia mtoto mlemavu anapaswa kulelewa kama mtoto yoyote asiye mlemavu.

Hapa nchini tunayo Sera ya Watu Wenye Ulemavu ambayo inatoa mwongozo na inaweka vigezo vya utoaji huduma na inalenga katika kuleta maendeleo, haki na heshima kwa Watanzania wenye ulemavu.

Kimataifa pia serikali imesaini mikataba mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu kama vile mikataba ya haki kwa watu wenye ulemavu (1975), Haki za Mtoto (1989) na Haki na Fursa Sawa kwa Watu Wenye Ulemavu (1993).

Hata hivyo pamoja na kuwapo kwa sera na kuridhiwa kwa mikataba mbalimbali ya kimataifa, bado kundi la watu wenye ulemavu linakabiliwa na changamoto mbalimbali huku zingine zikichangiwa na familia zenye watu wenye ulemavu.

Mratibu wa Watoto Walemavu kutoka Kijiji cha Magunga kilichoko Kata ya Mascati Wilaya ya Mvomero, Estela Kasian, anasema kijiji hicho kina jumla ya walemavu 11 na kati yao wawili ni walemavu wa akili na viungo.

Kasian anasema serikali ya kijiji haina utaratibu wa kufanya sensa ya walemavu waliopo kijijini hapo jambo linalochangia baadhi ya familia kuficha watoto wao ndani na hivyo kuwakosesha huduma muhimu.

Akitolea katika Kijiji cha Kipangilo wilayani Mvomero kuna mama alijifunga mtoto mlemavu lakini alikuwa hataki hata kumnyonyesha kwa kuogopa mpaka kufikia hatua ya mtoto huyo kufariki dunia kwa kukosa maziwa ya awali ya mama.

“Nilisikitishwa sana kwa mtoto yule kufariki na nilitoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya kijiji mama huyo apatiwe msaada kuweza kumlea mwanawe lakini nilikosa ushirikiano wa kutosha,” anasema Kasian.

Hata hivyo anaiomba serikali ya wilaya kupitia wataalamu wa afya kufika mara kwa sehemu za vijijini na kutoa elimu kwa jamii kuhusu walemavu, jinsi ya kuwalea na kuacha tabia ya kukaa ofisini na kufanya kazi kwa mazoea.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, Daniel Munga, anaeleza kuwa katika mpango kazi wa serikali ya kijiji hakuna utaratibu wa utambuzi wa watoto walemavu kutokana na kukosa bajeti na kukosa wataalamu.

Munga anasema kuwa familia nyingi zinakuwa na dhana potofu ya kuficha watoto ndani kutokana na kukosa elimu na kwamba wengi hawajui pa kuwapeleka kutokana na kukosa kipato cha kuwapeleka hospitali, matokeo yake huwaficha ndani mpaka wengine wanakuwa wazee kabisa.

Aidha anaiomba serikali kupitia wizara ya afya kunzisha vituo vya kulea watoto vijijini, kupeleka wataalamu kwa lengo la kusaidia kundi hilo lilosahaulika, walemavu wa mjini wanatambulika na kupewa misaada mbalimbali huku wa vijijini wakisahaulika.

Naye Mshauri wa Kituo cha Kulea Watoto Walemavu kilicho chini ya Mfuko wa Kumbukumbu wa Eric, Josephine Bakita, anasema wamekuwa wakitembelea nyumba kwa nyumba katika Wilaya ya Mvomero kuwatambua watoto wenye walemavu waliofichwa ndani na kuwapa wazazi elimu ya kuwahudumia watoto hao.

Anasema njia nyingine wanayotumia ni kuandaa semina kwa wazazi kwenye vijiji vyenye watoto wenye ulemavu, kuwaelimisha jinsi ya kuwalea na kwa wale wenye matatizo ya mtindio wa ubongo wazazi hushauriwa kuwapeleka katika vituo vya kulea watoto hao.

“Watoto wengi ninaowalea niliwapata baada ya habari kuelenea mtaani kuwa kuna taasisi ya kulea watoto wenye ulemavu imeanzishwa na inatoa malezi kwa watoto wasiojiweza na ambao wazazi wao hawataki watambulike,” anasema.

Pia anasema wakati mwingine huwatumia viongozi wa serikali za vijiji, kata na tarafa ambao wamekuwa wakipita kila nyumba kukagua kama kuna mtoto mwenye ulemavu na kumuandikisha kisha kumpeleka kwenye kituo cha kulea watoto wenye ulemavu.

Mshauri huyo anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika kuwatambua watoto wenye ulemavu ni usafiri kwani vijiji vingi vya Wilaya ya Mvomero viko mbali na si rahisi kuvifikika hivyo huwalazimu kutumia nguvu ya ziada ili kuwanusuru watoto hao.

Anasema familia nyingi zenye watoto walemavu haziwathamini watoto na hata inapotokea mtoto anaumwa huwa hapewi kipaumbele cha matibabu kama mtoto mwingine asiye na ulemavu.

Anafafanua kuwa familia nyingi zinaona mama kujifungua mtoto mlemavu ni mkosi kwa sababu wanategemea mtoto azaliwe akiwa amekamilika.

“Inapotokea tofauti wanakuwa na mshtuko na kuingiza imani za kishirikina. Sehemu zingine tunapita kutoa elimu ya kuwatambua walemavu na kupelekwa kwenye matibabu lakini viongozi wa vijiji wanapita kwa wananchi na kutoa kauli za kuwakatisha tamaa, kwamba watoto wao hawawezi kupata huduma yoyote ya afya jambo ambalo si sahihi,” anasema Bakita.

Anasema wakati mwingine mtoto mwenye ulemavu wa akili anapopelekwa hospitali kupata matibabu baadhi ya madaktari huwabeza na wengine hutoa kauli mbaya kwa walezi wa watoto hao jambo ambalo linatakiwa kukomeshwa ndani ya jamii.

Anasema watoto wenye ulemavu wa akili hawajiwezi kwa lolote, hawawezi kutoa sauti, hivyo wanapaswa kuangaliwa na si kutengwa ndani ya jamii.

Anaiomba serikali kuanzisha programu maalumu ya kuwatambua watoto wenye ulemavu wa akili kwa kila kijiji na kuweza kupewa huduma mhuhimu kwani wasipotambulika familia husika zitaona hawana faida kwao.

Mmoja wa wananchi wa Mvomero, Salum Mkolwe, anabainisha kuwa kinachosababisha wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani ni kushindwa kuwahudumia, umaskini, pamoja na kukosa shule maalumu za kuwapeleka, na hivyo kuona suluhisho pekee ni kuwaficha ndani.

Anashauri elimu iendelee kutolewa kwa umma kwa kusimamiwa na wizara husika, namna ya kuishi na wenye ulemavu na pia kuwafundisha kuepuka unyanyapaa kwa kuwa Tanzania inaamini binadamu wote ni sawa na wanahitaji huduma zote zinazostahili.

Pia anasema kuwa changamoto nyingine inayopelekea watoto walemavu kufichwa majumbani ni kutokana na baadhi ya jamii kuwa na imani potofu kwa kujiingiza katika masuala ya kishirikina na kuwafanya watoto wao misukule kwa tamaa ya kujipatia utajiri jambo ambalo linachangia watoto wengi kupoteza maisha.

Hata hivyo serikali inapaswa kuweka miundombinu rafiki katika kila eneo huku ikizingatia watu wenye ulemavu ili nao waweze kupatiwa huduma  kama ilivyo kwa wasio na ulemavu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles