25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

WFP: TANZANIA INAWEZA KUZALISHA CHAKULA CHA UKANDA WOTE WA AFRIKA

Na – MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasley amempongeza Rais John Magufuli kwa uongozi mzuri na kusema Tanzania inaweza kuwa mzalishaji wa chakula kwa ajili ya ukanda wote wa Afrika.

Amesema kwa kutambua hilo, shirika lake limedhamiria kutumia fursa hiyo kufanikisha mipango yake.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ilisema Beasley  ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku saba, aliyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Tumezungumza kuhusu namna Tanzania inavyong’ara kimataifa, kuhusu WFP inavyoweza kushirikiana na Tanzania kuboresha maisha ya wakulima wadogo, kupata masoko na bei nzuri ya mazao ya wakulima wadogo na tunaamini Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya ukanda wote wa Afrika.

“Hivyo tunataka kutumia fursa ya ukarimu, ushirikiano na uongozi bora wa Rais Magufuli na baraza lake la mawaziri ambalo tunaamini wamedhamiria kuboresha maisha, kuongeza tija na kuondoa rushwa,” taarifa hiyo ilimnukuu Beasley.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  Beasley alisema pamoja na kununua mazao ya chakula kutoka kwa wakulima kila msimu, WFP inaendesha miradi ya kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha mazao bora na kwa tija nchini Tanzania.

Alisema hivi sasa inao mpango wa kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya wakulima wanaofikiwa na mradi huo kutoka 50,000 hadi 250,000 katika miaka miwili ijayo.

Beasley aliahidi kulifanyia kazi ombi la Rais Magufuli la kutaka WFP iongeze kiwango cha mazao inayoyanunua kutoka kwa wakulima kutoka tani 56,000 za msimu uliopita, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya chakula cha ziada kinachozalishwa hapa nchini.

Ilisema Rais Magufuli naye alimpongeza Beasley kwa kutembelea Tanzania na dhamira yake njema ya kushirikiana na Tanzania katika kuwasaidia wakulima wadogo wa mazao ya chakula, kuongeza kiwango cha mahindi yanayonunuliwa na WFP na kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mazao na mizigo mbalimbali ya nchi za ukanda huu.

Rais Magufuli alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na WFP katika kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya ziada na kwamba katika msimu huu, Tanzania ina tani milioni nne za chakula cha ziada kinachopaswa kuuzwa nje ya nchi.

“Namshukuru sana kwa kuunga mkono juhudi tunazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, na hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha nchi inajikomboa kwa kuwa na uchumi wa kweli, tumedhamiria kujitegemea na namshukuru kwa kuunga mkono ‘Hapa Kazi Tu’ na juhudi zingine zote ikiwemo kupambana na rushwa,” taarifa hiyo ilimnukuu  Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles