27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wezi wa maji kushtakiwa Mahakama ya Mafisadi

Waziri wa Maji,  Gerson Lwenge
Waziri wa Maji, Gerson Lwenge

Christina Gauluhanga na Jonas Mushi, Dar es Salaam

SERIKALI imesema ipo haja ya kuwafikisha kwenye Mahakama ya Ufisadi watu wanaohujumu miundombinu ya maji.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Maji,  Gerson Lwenge alipotembelea Maonyesho ya 40 ya Sabasaba,  katika banda la Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA).

Alisema hadi kuwafikia wateja 400,000 mwishoni mwa Julai mwaka kesho maji yatakuwapo ya kutosha.

Alitoa mfano kuwa alipotembelea Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma alikuta mtu mmoja ameiba mabomba 40 na kusababisha watu wengi kukosa maji.

Lwenge  alisema huo ni uhujumu uchumi hivyo wanastahili kupelekwa Mahakama ya Ufisadi kwa vile  wanasababisha hasara kubwa kwa taifa.

“Usambazaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam ni mzuri ambako kuna wateja 250,000 lakini ni vema kufikia 400,000 Julai mwakani,” alisema.

Kuhusu upatikanaji wa maji,   Lwenge alisema miradi ya Ruvu chini na Ruvu juu imekamilika na unatoa maji kwa asilimia 100.

Alisema  Ruvu chini unatoa lita milioni 271 kwa siku huku Ruvu juu ukitoa maji lita milioni 913 kwa siku hivyo kufanya maji kuwa na nguvu  kubwa wakati wateja ni wachache.

Waziri alisema kwa sababu ya nguvu ya maji ya mabomba ambayo ni chakavu na hupasuka, mabomba mapya yameanza kufungwa.

Alisema   upotevu wa maji kwa sasa ni asilimia 35 tofauti na awali upotevu ulikuwa asilimia 50 huku viwango vya kimataifa vya upotevu wa maji vikiwa ni asilimia 30.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco,   Cyprian Luhemeja alisema   agizo la waziri litatekelezwa na   wateja watakopeshwa  maji kwa kujaza fomu maalum na kufungiwa  mita na kulipa kwa miezi 12.

Alisema hatua hiyo ilikuwa iishe Julai 30 mwaka huu lakini  muda umeongezwa hadi Julai 30 mwakani na akawakaribisha watu kufika kujaza fomu ili wafungiwe maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles