23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wenye mabucha waomba masharti nafuu kuuza nyama pori

Na Sheila Katikula,Mwanza

Wafanyabiashara wa mabucha ya nyama jijini Mwanza wameiomba Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kuweka masharti nafuu ili waweze kukidhi vigezo vya kuuza nyama pori.

Akizungumza kwenye kikao kazi cha kutoa elimu ya uanzishaji wa biashara ya nyama pori Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara wenye mabucha jijini hapa, Joshua Machage alisema ni vema mamlaka hiyo iweke masharti rafiki ili na wao waweze kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema kwa sasa Mamlaka hiyo inamtaka kila anayetaka kufungua mabucha hayo ya nyama pori ni lazima awe na bunduki ili aweze kuwinda mnyama anayemtaka jambo ambalo ni gumu kwao, wengi wao hakuna anayejua kupiga shabaha.

“Tunaiomba mamlaka hii itupunguzie masharti maana tumeambiwa ni lazima  umiliki bunduki ambayo ukiienda kwenye hifadhi  uweze kuwinda mnyama unaye mtaka, ni bora tulipe tozo ya kuwindiwa kwa sababu sisi hatuna utaalamu wa kupiga shabaha,” alisema.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa mabucha ya nyama, Manyama Bwire alisema kuanzishwa kwa utaratibu wa kuuza nyama pori ni fursa kwao lakini ili waweze kufungua mabucha hayo ni vema Mamlaka kupunguza masharti ikiwamo ya kuwinda kwenye mbuga ya Tabora kwani huku ni mbali tofauti na Serengeti ni karibu na mkoani hapa. 

“Naiomba serikali itupe vitalu vya karibu tofauti na kwenda Tabora ni mbali na kanda ya magharibi kwanini wasitupeleke kwenye hifadhi ya Serengeti ndiyo karibu na mkoa wetu.

“Tumeambiwa ni lazima kwenye bucha anayeuza awe na elimu ya kidato cha nne na mwenye ujuzi wa kuchakata nyama aliyesomea chuo cha ufundi lakini kwenye mabucha mengi watu wanafanya kazi kwa uzoefu tu kwanini  wasituache kama tulivyozoea ili watu waweze kupata ajira,”alisema Bwire.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba aliwataka  wafanyabiashara hao kuhakikisha wanachangamkia fursa hiyo sanjari na kufuata masharti ya Mamlaka hiyo ili waweze kukidhi vigezo  vilivyowekwa na Wizara hiyo.

Aidha Ofisa Uhifadhi wa Wanyamapori, Hilda Mikongoti alisema ni vema wafanyabiashara hao kufuata sheria zilizowekwa ili waweze kufanya shughuli zao bila usumbufu.

Hata hivyo, Ofisa Utalii Idara ya Utalii Kanda ya Ziwa, David Kasito alisema kila mfanyabiashara anayetaka kufungua bucha la wanya mapori anawajibu wa kufuata sheria na utaratibu za wizara hiyo sanjari na kuwataka wananchi wajitokeze  kuchamkia fursa hiyo ili waweze kutoa ajira kwa watu kwenye ujuzi wa kuchakata nyama na kukuza uchumi.

Kwa upande wake Ofisa Wanyamapori kutoka kikosi dhidi ya ujangili  (KUD) Mwanza Laurent Yohana alisema ili kuweza kufungua bucha la kuuza nyama hizo ni lazima kuwe na msumeno wa kukatia, kitabu cha mauzo, risiti, mashine ya EFD, jengo likikidhi vigezo, muuzaji ni lazima awe na elimu ya kidato cha nne na kwenye ujuzi wa kuchakata nyama ambaye amesomea chuo cha ufundi.

“Mfanyabiashara akikidhi vigezo vyote  atalipia ada ya usajili ya miaka mitano  Sh 250,000 na atapewa leseni ya biashara ya nyaraka daraja la 21 tunafanya hivi ilikufunguza  ujangili.

“Sisi kazi yetu ni kumuonyesha aina ya mnyama anayemtaka, kupiga shabaha ni jukumu lake, nyati atanunua kwa sh milioni moja, ambaye ana kilo 800 akitolewa kila kitu anabaki na kilo 600  bei ya kuuza kwa wateja  atapanga yeye”,alisema Yohana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles