Dawati la jinsia Arusha latoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi Chuo cha Ufundi Arusha

0
383

Na Janeth Mushi, Arusha

Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na vya Kati wametakiwa kutokuficha taarifa za vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia vinavyotokea katika maeneo yake na badala yake kutoa taarifa.

 Kauli hiyo imetolewa  leo Desemba 30, 2020 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha, ASP Happiness Temu, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha kuhusiana na masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao katika kikao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho.

Mlezi wa wanafunzi Stella Ngowa (aliyekaa katikati), rais wa serikali ya wanafunzi katika chuo cha ufundi Arusha (aliyevaa koti jeusi), Issa Mohamed, wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa katika kikao kilichojadili masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu unaohusisha makosa ya mitandao kilichofanyika katika bwalo la chuo hicho jijini Arusha.

Amesema kuwa ngazi ya chuo ni sehemu muhimu yenye jamii kubwa ya wanafunzi ambao wametoka maeneo mbalimbali na kukutana ndani ya chuo wakiwa na tabia tofauti, hivyo kutokana na tabia hizo vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa  wanafunzi wamekuwa na aibu kuvieleza.

‘‘Wapo baadhi ya wanafunzi wanawafanyia wenzao vitendo vya kikatili na wanaona ni mambo ya kawaida na wale wanaofanyiwa ukatili wanaumia lakini kwa hofu wanaogopa kusema au  hawaelewi ni wapi wanaweza kupeleka malalamiko yao.

“Tunawaasa wawe na uwezo wa kujieleza kwa sababu kuwa na jamii ya wasomi ambao ni waoga wa kujieleza kuhusiana na vitendo vya ukatili ama kuona aibu ni vibaya, hivyo tumefika hapa ili kuwajengea uelewa na uwezo ili waweze kutoka na kukemea vitendo hivyo kwenye jamii,” amesema ASP Happiness.

Amesema ili kuweza kuisaidia jamii, ni wakati sasa wa kutengeneza watu ambao watatoka vyuoni wakiwa bora na wasiopenda masuala ya ukatili na wenye uwezo wa kukemea, hivyo waliona ni vyema elimu hiyo waitoe katika maeneo ya vyuo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Issa  Mohamed,alishukuru Jeshi la polisi mkoa wa Arusha kupitia kitengo cha dawati la jinsia na watoto kwa elimu  waliyoitoa kuhusiana na masuala ya ukatili na uhalifu unaotokana na matumizi mabaya ya mitandao.

Amesema elimu hiyo imekuja katika muda muafaka kwakuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanatumia mitandao na hawana uwelewa kuhusu uhalifu wa kimtandao pamoja na masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambapo watahakikisha elimu hiyo inawafikia wanafunzi wote chuoni hapo.

‘‘Kama wanafunzi tutaangalia ni namna gani tunahamasishana ili kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na matumizi mabaya ya mitandao ambayo inaweza kutupelekea katika makosa ya uhalifu wa mitandao,” amesema ASP Happiness.

Amesisitiza kwa kuwa wanafunzi wanatoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, anaimani elimu waliyoipata itasambaa maeneo yote kwani watakuwa mabalozi wazuri wa kuieleza jamii kuepukana na makosa hayo.

Huu ni mwendelezo wa elimu ambazo dawati hilo la jinsia na watoto mkoa wa Arusha linatoa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni, vyuoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusiana vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here