Aveline Kitomary, Dar es salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo amethibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya corona ambaye ni mwanamume aliyekuwa akitibiwa katika kituo cha matitabu ya wagonjwa wa corona kilichopo nje ya hospitali ya Mloganzila.
Waziri Ummy amesema mgonjwa aliyepoteza maisha ni Mtanzania mwenye umri wa miaka 49 aliyekuwa akipatiwa matibabu katika kituo hicho.
“Nasikitika kutangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Covid -19 hapa nchini kilichotokea alfajiri ya leo tarehe Machi 31, wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Mloganzila Dar es salaam.
“Marehemu ni Mtanzania mwenye umri wa miaka 49 ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine, tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi na tunatoa pole kwa ndugu hasa wa marehemu,” amesema Waziri Ummy.
Hadi sasa jumla ya wagonjwa waliopata maambukizi ya Covid-19 nchini ni 19, aliyepona ni mmoja na aliyefariki dunia ni mmoja.