25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watu 200,000 huenda wakafa kwa corona Marekani

WASHINGTON, MAREKANI

RAIS wa Marekani, Donald Trump ameongeza muda wa vizuizi vya dharura katika kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona ambako wanasayansi wanaonya kwamba huenda hadi watu 200,000 wakafa kwa maradhi ya Covid-19.

Rais Trump pia ameongeza muda wa watu kujitenga na mijumuiko hadi Aprili 30, akiachana na muda wa awali aliouweka wa zuio hilo ulioishia wakati wa sherehe za pasaka.

“Kwa hiyo kwa wiki mbili zijazo na katika kipindi hiki chote ni muhimu kwa kila mmoja kufuata kikamilifu miongozo, ambayo makamu wetu wa rais anaisisitizia sana. Ana iamini sana, kadiri tunavyofanya kwa haraka, ndivyo tutasaidia kulimaliza haraka  jinamizi hili. Kwa hiyo, tutaongeza muda wa miongozo yetu hadi Aprili 30 ili kupunguza kasi ya maambukizi,” alisema Trump.

Hatua hii ya Trump inakuja wakati ambapo Uingereza na Italia ambayo imeathiriwa pakubwa na virusi vya corona zikionya kwamba hatua za kupambana na kusambaa zaidi kwa virusi hivyo zitadumu kwa miezi kadhaa inayokuja, huku akionya kwamba mzozo huo utaendelea kuiathiri vibaya Marekani.

Idadi ya watu walioambukizwa inakaribia 700,000 ulimwenguni kote.

Covid-19 tayari imewaua watu zaidi ya 33,000 kote ulimwenguni, huku idadi ya visa vilivyothibitishwa ikikaribia 700,000.

Nchini Ujerumani, taasisi ya masuala ya afya ya umma na udhibiti wa magonjwa ya Robert-Koch imeeleza kuwa idadi ya walioambukuzwa imeongezeka hadi 57,298, baada ya kugunduliwa visa vipya 4,751. Vifo 66 vilivyoripotiwa vimefanya idadi ya waliokufa sasa  kufikia 455.

Jiji la Moscow nchini Urusi limeanza utekelezaji wa amri ya kusimamisha shughuli kufuatia tangazo la ghafla la sheria mpya za meya wa jiji la hilo usiku kuamkia jana.

Meya Sergei Sobyan alitangaza sheria hizo baada ya wakazi wa kupuuza ushauri rasmi wa kujitenga na mijumuiko katika siku za mwisho wa wiki.

Watakaoruhusiwa ni wafanyakazi wa shughuli zitakazotambuliwa kuwa muhimu, wanaotoka kununua vyakula na dawa na shughuli nyingine muhimu, lakini si umbali wa zaidi ya mita 100 kutoka kwenye makazi yao.

India pian imesema haitaogeza muda wa kusimamisha kabisa shughuli nchini humo, hii ikiwa ni kulingana na tangazo la Serikali ya nchi hiyo jana.  

Hatua yake hiyo iliyoshuhudia watu bilioni 1.3 wakishindwa kufanya shughuli za kila siku ili kujikimu inahitimishwa Aprili 15 wakati kukiwa na visa 1,071 na vifo 29.

Nchini Israel, msaidizi wa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu amekutwa na maambukizi ya virusi hivyo, hatua inayoiweka mashakani afya ya waziri mkuu huyo mwenye miaka 70. Hata hivyo vyombo vya habari vimesema msaidizi huyo anaendelea vizuri.

Huku hayo yakiendelea, huko Belarus, Rais Alexander Lukashenko amepuuzilia mbali janga la corona na hata kuwahimiza watu wake kuendelea na biashara kama kawaida, akidai kwamba shughuli zinazofanywa kwa kutumia matrekta mashambani zina uwezo wa kuwasaidia wakulima kupona na janga hilo.

RWANDA YATANGAZA MAAMBUKIZI MAPYA

Rwanda imethibitisha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa watu 10 zaidi siku ya Jumapili na kufikisha 70 jumla ya watu wanaougua corona, Wizara ya afya Rwanda imetangaza.

Katika hotuba yake kwa Taifa usiku wa Ijumaa, Rais Paul Kagame alisema idadi hiyo itaendelea kuongezeka kwa sababu wale waliotangamana na waathirika wanaendelea kutafutwa.

Katika visa vya hivi punde vya maambukizi, watu sita walitokea Dubai, wawili kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Nigeria na mwigine alikuwa amesafiri maeneo ya Afrika mashariki hivi karibunii, ilisema taarifa ya wizara ya afya nchini humo.

Rwanda kwa sasa in ajumla ya wagonjwa 70 wa corona, 32 kati ya hao waliwasili nchini kutoka Dubai.

Wiki iliyopita Waziri wa Afya wa Rwanda alikiambia kituo cha televisheni cha Rwanda kwamba hali hiyo ya maambukizi ilitokea baada ya wafanyibishara wengi wa Rwanda kurejea nyumbani kutoka Dubai, serikali ilipotangaza kuwa itafunga mipaka yote ya nchi.

Rwanda inaongoza kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa corona katika kanda ya Afrika Mashariki ikiwa na wagonjwa 70, ikifuatiwa na Kenya 42, Uganda 33, Tanzania 14, huku Burundi na Sudan Kusini zikiwa hazijarekodi visa vyovyote vya maambukizi.

Siku ya Jumapili Rwanda ilianza wiki ya pili ya kukaa nyumbani ili kudhibiti kuenea kwa virusi.

Katika hotuba yake kwa Taifa, Kagame alisema Serikali inatoa msaada wa chakula kwa kwa familia zisizojiweza na ambazo zimeathiriwa na amri ya kukaa nyumbani.

Mamlaka nchini humo siku ya Jumamaosi alianza shughuli ya kugawa chakula mjini Kigali kwa kuzitambua familia masikini zinazojikimu kutokana na shughuli za kila siku.

Maelfu ya familia zinatarajiwa kupokea vyakula vya msaada kutoka kwa serikali mchakato wa utambuzi utakapokamilika.

Mwanzoni mwa juma lililopita, Rwanda ilitangaza kufunga mipaka yote ya nchi hiyo na watu kuamrishwa kusalia majumbani mwao katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na watumishi wote wa serikali na wa kibinafsi kufanyia kazi nyumbani na safari za kuenda mikoani kusitishwa kwa wiki mbili kukiwa na uwezekano wa muda huo kuongezwa.

Vilabu vya pombe na, maduka yasio ya chakula pia yamefungwa huku usafiri wa bodabobda ukisitishwa.

Hatua hiyo ilichukuliwa siku moja baada ya wizara ya afya ya Rwanda siku ya Jumamosi kutangaza kuwa watu wengine sita wameambukizwa virusi vya corona miongoni mwao mtoto mchanga wa miezi 10.

KENYA YAZINDUA MPANGO WA KUPIMA

Wizara ya Afya ya Kenya imeanza kufanya upimaji wa ugonjwa wa Covid-19 au corona kwa watu wote walioingia nchini humo wiki iliyopita na wale waliowekwa karantini kwenye vituo vya serikali au hoteli zilizoteuliwa.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema, upimaji huo utafanyika kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu upimaji wa corona, na kulingana na tarehe ya kuwasili kwao.

Kagwe pia amesema kutokana na hatari ya corona, na shinikizo kubwa kwa raslimali za huduma za afya, ni muhimu kwa serikali kuwalazimisha watu waliothibitika na wale waliokaribiana nao kuwekwa kwenye karantini.

Vilevile amewataka Wakenya kuzingatia usafi binafsi kwani ni msingi wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19. Hadi sasa watu 42 wameambukizwa corona nchini Kenya huku mtu mmoja akifariki na mwingine akipata nafuu.

Hadi sasa Serikali ya Kenya imewapima watu 1,141 na miongoni mwao 163 wameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya karantini ya siku 14 huku wengine 978 wakiendelea kufanyiwa uchunguzi baada ya kukutana na watu waliokuwa na corona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles