Na Amina Omari, Tanga
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu ametoa msaada wa mifuko 600 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni 8.4 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari zilizopo kwenye Halimashauri ya Jiji la Tanga.
Msaada huo ametoa jana Desemba 27, baada ya kufanya ziara katika shule za tisa za sekondari ambazo zinatarajia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Januari 2021 ilo kujionea hatua za utekelezaji wa ujenzi huo
Ummy amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo inayofanywa na Halimashauri kwa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha lengo la serikali la wanafunzi wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wanaanza masomo kwa wakati.
“Kama mbunge nimefurahishwa na juhudi zinazofanywa na wananchi katika kusaidia Serikali yao lakini katika kuweka mazingira wezeshi ya watoto wao kupata elimu, niwaahidi kusaidia juhudi hizo kwa hali na mali,” amesema Ummy.