Na Damian Masyenene, Shinyanga
Watumishi wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani hapa ambao wanadaiwa kuwa sehemu ya kukwama na kushindwa kukamilika kwa machinjio ya kisasa iliyopo Ndembezi mjini Shinyanga, wamesimamishwa kazi kwa muda wa wiki mbili kupisha uchunguzi kwa tuhuma zinazowakabili.
Watuhumiwa hao ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mifugo, Dk. Tito Kagize ambaye kwa sasa amehamishiwa manispaa ya Morogoro, Mchumi wa Manispaa, Gwakisa Mwakyebwa, injinia ujenzi wa halmashauri hiyo,Kassim Thadei na aliyekuwa mkuu wa idara ya manunuzi, Godfrey Mwangailo ambaye sasa yupo halmashauri ya Kigamboni, Dar es Salaam ambao wote wanadaiwa kushindwa kutimiza wajibu wao kwa kutochukua maamuzi na kuishauri halmashauri kutokana na mwenendo usioridhisha wa mradi huo.
Maamuzi hayo yamefikiwa Mei 28, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu baada ya kufika katika machinjio hiyo akiwa katika ziara yake mkoani Shinyanga, ambapo mbali na kusimamishwa kazi kwa watendaji hao, ameagiza pia watolewe kwenye vituo vyao vya sasa vya kazi na warejeshwe Shinyanga kwa ajili ya kujieleza.
Mbali na wakuu hao wa idara, Waziri Ummy pia ameitaka halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuwaandikia barua Mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya Home Africa pamoja na Mhandisi Mshauri, B.J Amour na wapelekwe Bodi ya Mkandarasi (CRB) ili iwawajibishe na wajieleze.
“Mradi huu haukusimamiwa vizuri na tunawatesa watu wa Shinyanga, mpaka leo haujakamilika na fedha hazionekani, kuna Sh milioni 800 zimelipwa kwa wakandarasi bila kuhakikiwa wala kujiridhisha. Huu mradi ni aibu kwa Shinyanga na ni kashfa kwa watendaji wa Manispaa. Kwahiyo nawasimamisha hao kwa wiki mbili ili wapishe uchunguzi.
“Wakae pembeni wiki mbili wapishe uchunguzi. Mkuu wa mkoa mlisimamie mtoe haki na mnipe taarifa, huu mradi lazima ukamilike,” amesisitiza.
Machinjio hiyo ilianza kujengwa mwaka 2018 na ilitazamiwa ikamilike mwaka 2019 na kuanza kutoa huduma, lakini maendeleo yake yamekuwa yakisuasua na kusababisha baadhi ya viongozi kuilalamikia akiwemo Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi ambaye alimuomba aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jaffo kuchukua hatua na kufanya uchunguzi kwenye mradi huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amesema kuwa mradi huo ulitengewa Sh bilioni 5.7 lakini hadi sasa zimetumika Sh bilioni 5.1 na Sh Milioni 600 hazijulikani ziko wapi wakati mradi haujakamilika, ambapo amesisitiza kuwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilieleza kuwa kwenye mradi huo kuna ufisadi na haukutekelezwa vizuri.
Hatua hiyo ya Waziri Ummy umekuja baada ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila ambaye pia ni diwani wa Kata iliko machinjio hiyo, kueleza kuwa kamati ya fedha ya halmashauri hiyo kupitia baraza la madiwani walikuwa wameanza kuchukua hatua baada ya kubaini kuwa thamani ya fedha katika mradi huo haikuwa sawa, huku akibainisha kuwa kupitia vyanzo vya ndani watatenga Sh Milioni 172 kwa ajili ya kukamilisha machinjio hiyo.
“Kupitia kamati ya fedha tulikwishaelekeza na kuchukua hatua za awali ikiwemo kuwachaji na kutakiwa kujieleza watendaji akiwemo Mchumi, Mkuu wa idara ya Mifugo, Injinia wa Halmashauri, PMU (manunuzi) na mshauri B.J Amour ambaye aliona makosa lakini hakutushauri na Contractor Home Africa naye ni miongoni mwa wanaopaswa kutupa maelezo ya sakata hili.
“Naungana na wewe na hata madiwani wanaungana na wewe, tutafanya jitihada zote kuhakikisha mradi unanufaisha wananchi kadri ulivyotazamiwa,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati amesema kuwa amepokea maelekezo ya Waziri na kwamba yatafanyiwa kazi na kusimamiwa vizuri na haki itatendeka ili wote waliochezea rasilimali za umma wawajibike.