Na Samwel Mwanga
WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza achukuliwe hatua daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Laurent Biyengo, aliyedaiwa kushindwa kuingia kazini badala akaenda kunywa pombe.
Inadaiwa kuwa kitendo hicho kilisababisha wagonjwa kutopatiwa huduma za utabibu.
Waziri alitoa maelekezo hayo kwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dk. Zainab Chaula, hivi karibuni.
Inaelezwa kuwa baadhi ya wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo Septemba 27 mwaka huu saa 1:00 hadi saa 3:30 usiku walikosa kukosa huduma kwa vile daktari huyo wa zamu hakuwapo.
Hali hiyo ilisababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John kuharibika wakati wakimsubiri daktari huyo ambayo ilidaiwa alikuwa anakunywa pombe.
Waziri Ummy aliutoa maelekezo hayo kwa simu baada ya kupata taarifa hizo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka kwa mwandishi wa MTANZANIA kuhusu kutokuwapo daktari wa zamu hospitalini hapo.
“Nimemwelekeza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi ashughulikie suala hilo,” alisema Waziri.
Wagonjwa waliopatwa na madhira hayo walisema walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu lakini cha kushangaza daktari wa zamu hakuwapo.
Kwa mujibu wa wagonjwa hao, wauguzi waliokuwapo walishindwa kumhudumia hasa Salome John aliyekuwa akilia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata.
Wauguzi hao walisema taratibu zilikuwa haziruhusu hadi waelekezwe na daktari hali iliyosababishaujauzito wa mgonjwa utoke.
“Tulimsubiri daktari lakini hakuonekana na ilipofika saa 3:20 usiku maumivu yalimzidi binti yangu na hatimaye mimba yake ikatoka,” alisema Suzana Kalumbilo ambaye ni mama mzazi wa Salome John.
Walieleza kuwa baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walimpigia simu Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Seif Shekalaghe ambaye naye alichukua jukumu la kumpigia simu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk. Jonathan Budenu.
Dk. Budenu alifika muda mfupi baada ya kupigiwa simu na DC Dk. Shekalaghe na kufanya jitihada za kupata daktari mwingine ambaye alifika na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa waliokuwapo, walisema wagonjwa hao.
Walisema Ilipofika saa 3:40 usiku ndipo Bihengo alipofika akiwa amelewa lakini Dk. Budemu alimtoa nje na kumtaka asitoe huduma yoyote kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk .Shekalaghe alisema amesikitishwa na kitendo hicho na kueleza kuwa hawezi kuwavumilia watumishi wa serikali wa namna hiyo.
Alisema watumishi wa aina hiyo wamekuwa wakiichonganisha serikali na wananchi kutokana na kutotimiza majukumu yao.
Hata hivyo aliulaumu uongozi hospitali hiyo kwa kushindwa kuwasimamia watumishi wa aina hiyo.