NA ESTHER MNYIKA ,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maliasili na Utalii , Profesa Jumanne Maghembe ameishauri Serikali kuangalia upya endapo bado kuna sababu za msingi kwa wananchi kuendelea kununua na kumiliki bunduki zenye mitutu mikubwa.
Ametoa ushauri huo kutokana na kuongezeka matukio ya kukamatwa kwa silaha zikiwa zinatumika katika vitendo vya uhalifu nje ya mikono ya wamiliki halali wa silaha hizo.
Mbali na Profesa Maghembe, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema umefanyika uchunguzi na kubaini wanaomiliki silaha wanazikodisha kwa majangili.
Alisema jeshi la polisi linatarajia kuendesha operesheni maalum nchi nzima kwa lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya silaha kwa wananchi wanaozimiliki.
“Miaka iliyopita wananchi walikuwa waaminifu… kwa sasa baadhi baadhi yao wanaihujumu Serikali kwa kufanya biashara ya kukodisha silaha kwa majangili,”alisema IGP Mangu.
Profesa Maghembe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Waziri pia aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu uliosaidia kukamata majangili wanaodaiwa kuhusika na tukio la kutunguliwa helikopta ya doria Januari 29 mwaka huu.
Majangili hao wanadaiwa kushambulia helikopta iliyokuwa inafanya doria katika pori la akiba Maswa na ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba.
Tukio hilo lilisababisha kifo cha rubani Rogers Gower raia wa Uingereza huku Nick Desta aliyekuwa pamoja na Rogers akinusurika na kukumbizwa Nairobi kwa matibabu .
Profesa Magembe alisema tukio hilo limetoa funzo kubwa kwa nchi na linadhihirisha kwamba baadhi ya majangili wamefika hatua ya kujijengea uthubutu na ujasiri wa kutisha.
“Kutokana na mazingira hayo wizara yangu imeamua kurejea kwa haraka na kwa upana zaidi mbinu na mikakati yake dhidi ya ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori,” alisema.
Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha na kuunda haraka kikosi maalum cha kupambana na uhalifu wa wanyamapori.
“Kikosi hiki kitaundwa kwa kushirikiana na taasisi zote za wizara kama Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Wnyamapori Tanzania (TAWA), Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),” alisema Waziri Maghembe.
Alisema kuanzia sasa majangili watatafutwa kwa kutumia teknolojia akisisitiza kuwa hakuna operesheni tokomeza tena.