23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mtanzania auawa kwa mawe Kenya

Japheth-KoomeMwandishi Wetu na Mashirika ya Habari

MTANZANIA ameuawa kwa mawe na watu wenye hasira jijini Nairobi baada ya kuwashambulia na kuwaua watumishi wawili wa casino, ambamo alipoteza fedha alipocheza kamari.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema mwanamume huyo ambaye vyombo vya habari vimemtambua kama John Barnabas Mchanga, alikuwa amepoteza dola 300 sawa na zaidi ya sh 600,000 za Tanzania akicheza kamari.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia, Mtanzania huyo alijaribu kumsihi msimamizi wa casino hiyo aruhusiwe kuweka rehani simu yake, lakini akakatazwa kwa msingi kuwa haikuwa imefikisha thamani ya kuwekwa rehani.

Mkuu wa Polisi jijini Nairobi, Japheth Koome ameripotiwa akisema kuwa taarifa walizonazo ni kwamba Mtanzania huyo alimshambulia kwa kisu na kumuua meneja wa kike wa casino hiyo, ambaye alikataa kumkopesha fedha ili aendelee kucheza kamari.

“Kisha akamchoma meneja ulinzi, ambaye alijaribu kuingilia kati na akamuua,” Koome alikaririwa akisema.

Mlinzi mwingine alijeruhiwa vibaya katika shambulio hilo, ambalo lilitokea muda mfupi baada ya usiku wa manane na alikimbizwa katika hospitali jirani.

“Wakati maofisa wa polisi walipowasili walimkuta amekufa,” Koome aliwaambia wanahabari na kuongheza kuwa uchunguzi umeanzishwa kuchunguza tukio hili.

Tukio hilo awali lilisababisha mshtuko na vurugu katika casino hiyo ya City View Bar and Restaurant ambapo watu walikimbia kuokoa maisha yao, huku kundi jingine la watu lililokuwa likifuatilia mchezo likimkabili mcheza kamari huyo.

Kundi hilo lilimkimbiza Mtanzania huyo na kumpiga mawe hadi kufa mtaani.

Polisi waliwasili eneo la tukio wakiwa wamechelewa na kuwahoji walioshuhudia mapema jana asubuhi.

Aidha polisi walisema mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 28 anatoka eneo la Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania.

Kwa mujibu wa wanaomfahamu, alikuwa akifanya kazi kama fundi wa viatu kabla ya kuanza biashara ya bodaboda.

Kabla ya kisa hicho, waliokuwa wakifanya kazi naye walisema kuwa alikuwa ameiuza bodaboda hiyo.

Uchezaji kamari umejipatia umaarufu jijini Nairobi katika miaka ya karibuni na casino kwa sasa ziko karibu kila mtaa wa jiji hilo. Mapato kutokana na casino mwaka 2014 yaliripotiwa kufikia dola milioni 20 kwa mwaka, likiwa ongezeko la zaidi ya asilimia sita.

Hata hivyo, ukuaji wa mapato kutokana na kamari unatarajia kuanguka kutokana na kupungua kwa ukuaji wa uchumi kwa mujibu wa ripoti ya kitaalamu ya Kampuni ya Pricewaterhouse Coopers.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles