Na ELIUD NGONDO,
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula, amesema mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wilayani Momba, ni tofauti na mipaka mingine baada ya kuvamiwa na makazi.
Mabula aliyasema hayo alipotembelea jana mpaka huo akisema umekuwa na ramani ambazo hazieleweki.
Alisema mpaka huo umekuwa na mwingiliano mkubwa na kujengwa nyumba za makazi na taasisi mbalimbali likiwamo kanisa moja lililojengwa katika ya mpaka bila kuzingatia alama.
“Ili kuutengeneza vizuri mpaka huu ni lazima nyumba zote zilizo ndani ya mita 60 zivunjwe kwa pande zote, Tanzania na Zambia na baada ya hapo sasa kutakuwa na ramani inayoeleweka,” alisema Mabula.
“Yanahitajika mazungumzo ya ngazi ya juu kwa nchi zote mbili.
“Mazungumzo yakiamuriwa kwa pamoja hatua ya kuvunja nyumba na kuuweka mpaka vizuri itafanikiwa bila matatizo,” alisema Mabula.
Mkuu wa Wilaya ya Momba ,Juma Irando, alisema mwingiliano wa makazi katika mpaka huo limekuwa ni tatizo.
Alisema hata masuala ya ulinzi ni magumu kutokana na wananchi kujenga nyumba zao ndani ya mpaka huo.
DC alisema hata ukusanyaji wa mapato nao ni tatizo kutokana na wafanyabiashara wengi kufanya shughuli zao Zambia wakati ni watanzania.
“Mpaka huu limekuwa ni tatizo hata maofisa wa ukusanyaji wa mapato wakija wafanyabiashara wanaenda upande wa Zambia… ukimkamata anasema yeye ni Mzambia na katika sheria anakushinda,” alisema Irando.
Mkuu huyo alisema umekuwapo mwingiliano mkubwa wa wananchi ambao wamekuwa wakifanya biashara na wengine wakiwa wamejenga makazi yao Zambia kwa kutokutambua mpaka.
Baadhi ya wananchi walisema suala la mpaka huo limekuwa ni tatizo kutokana na alama zake kutokuonekana vizuri na mwingiliano wa makazi umezidi kuongezeka.
Juma Mgala, mkazi wa Tunduma alisema serikali zikikubaliana kuutengeneza mpaka huo itakuwa ni manufaa makubwa hata vitendo vya uhalifu vitapungua