27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

VYANZO VIFO VYA WACHEZAJI UWANJANI VYATAJWA

Mwili wa aliyekuwa mchezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Mbao FC , Ismail Mrisho Khalfan, ukishushwa nyumbani kwao mtaa wa Uhuru jijini Mwanza jana kwenda kuzikwa ukitokea mkoani Kagera alipofariki akicheza uwanjani na timu ya Mwadui.
Mwili wa aliyekuwa mchezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Mbao FC , Ismail Mrisho Khalfan, ukishushwa nyumbani kwao mtaa wa Uhuru jijini Mwanza jana kwenda kuzikwa ukitokea mkoani Kagera alipofariki akicheza uwanjani na timu ya Mwadui.

Na WAANDISHI WETU,

MADAKTARI wa tiba za michezo nchini, wameeleza kuwa mshtuko wa moyo, furaha ya kupitiliza na huzuni ndiyo sababu zinazochangia matatizo ya afya kwa wachezaji uwanjani na kuwasababishia vifo.

Kauli hiyo inatokana na tukio la kusikitisha lililotokea juzi katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, baada ya mchezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Mbao FC, Ismail Mrisho, kufariki ghafla uwanjani.

Ismail (19) alipoteza maisha juzi jioni baada ya kuanguka uwanjani dakika ya 74 ya mchezo, ikiwa ni muda mfupi tangu aifungie timu yake bao la kuongoza katika mchezo wa ligi ya vijana ya U-20 dhidi ya Mwadui FC.

Kufuatia tukio hilo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeunda Kamati ya Tiba ili kufanya uchunguzi wa kifo cha mchezaji huyo ambaye alizikwa jana katika Makaburi ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.

Mazishi ya Ismail ambaye alimaliza kidato cha nne mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Mwanza, yaliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Akizungumzia kifo hicho, Katibu Msaidizi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA), Shecky Mngazinja, alisema zipo sababu nyingi zinazosababisha vifo vya wachezaji uwanjani, huku akidai Ismail huenda aligongwa sehemu isiyo sahihi.

Mganzija alisema kifo kinaweza pia kutokea kama furaha au huzuni imezidi sana kwa kuwa kitaalamu kila kitu kinatakiwa kiwe kwa kiasi na kuongeza kuwa mara nyingi vifo vya namna hiyo vinatokea sana michezoni.

Alisema kwa sheria ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Shirikiho la Soka Afrika (CAF) na TFF, inashauriwa uchuguzi wa afya ya wachezaji kufanyika kabla ya mashindano ili kusaidia kutambua maradhi na utimamu wa mwili na akili kwa sababu kama mchezaji ana maradhi ambayo hayajagundulika, huenda ikasabisha kifo cha ghafla.

“Kupima afya ni jambo la msingi kwani wataalamu wanaangalia utimamu wa mwili na akili kwa sababu inawezekana mchezaji anaposumbuliwa na tatizo la mapafu, figo au ini na akafanya mazoezi kwa kiwango fulani, inaweza kuzidisha au kupunguza tatizo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha straika huyo tegemeo wa timu ya Mbao, wakati wa kuaga mwili wa marehemu jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kagera.

“Serikali inaungana na ndugu na jamaa wa marehemu katika kipindi hiki kigumu, tumetoa usafiri ili uweze kusafirisha mwili wa marehemu hadi jijini Mwanza kwa ajili ya mazishi,” alisema Kinawilo.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL), Boniface Wambura, alisema jukumu la kuwafanyia vipimo vya afya wachezaji kabla ya usajili linatakiwa kufanywa na klabu zenyewe.

Alisema TFF haitoi leseni ya usajili kwa mchezaji hadi awe amefanyiwa vipimo vya afya na kupata cheti cha vipimo vyake ambacho hutumika kumuombea usajili mchezaji husika.

Tukio jingine la mchezaji kupoteza maisha uwanjani lilitokea Juni 26, mwaka 2003 kwa mchezaji wa Cameroon, Marc Vivian Foe, ambaye alianguka wakati akiitumikia timu yake ya taifa katika michuano ya Kombe la Shirikisho hatua ya nusu fainali dhidi ya Colombia.

Pia Januari 25, mwaka 2004, nyota wa klabu ya Benfica, Miklos Feher, alipoteza maisha uwanjani baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo wakati timu yake ikicheza dhidi ya Victoria.

Agosti 30, mwaka 2006, mchezaji wa timu ya Al Ahly ya nchini Misri, Mohamed Abdelwahad, alipoteza maisha akiwa mazoezini na timu yake wakati wa kujiandaa na mechi ambapo ilidaiwa alipata mshtuko wa moyo.

Pia nyota wa klabu ya Sevilla ya nchini Hispania, Antonio Puerta, alianguka uwanjani Agosti 28, mwaka 2007, katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Gatafe FC, lakini alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo baada ya kufikishwa hospitali.

Machi 6, mwaka 2010, mchezaji wa klabu ya EL Merreikh ya Sudani, Endurance Idahor, alipoteza maisha akiwa kwenye gari akipelekwa hospitali baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa mchezo dhidi ya Alamal Atbara na Mei 6, mwaka 2016, kipa wa timu ya Taifa ya wanawake ya Cameroon, Jeanine Christelle, alipoteza maisha uwanjani kwa tatizo la mshtuko wa moyo wakati timu hiyo ikifanya mazoezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles