24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu Majaliwa aapishwa

maj1NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Kassim Majaliwa kuteuliwa na Rais John Magufuli na kuthibitishwa na Bunge kwa asilimia 73.5 kuwa Waziri Mkuu, jana aliapishwa kuanza kazi rasmi katika wadhifa huo.

Majaliwa, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, aliapishwa na Rais Magufuli majira ya asubuhi katika sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Ikulu ndogo ya Chamwino, mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakuu wa vyombo vya ulinzi pamoja na viongozi wastaafu.

Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na watu wa kada mbalimbali, wakiwemo viongozi na wanasiasa, pia lilihudhuriwa na familia ya Majaliwa, ikiongozwa na mke wake, Mary Majaliwa, watoto wake pamoja na ndugu wengine.

Majaliwa alikula kiapo chake cha uaminifu mbele ya Rais Magufuli akiwa ameshikilia Msahafu na kusoma mwongozo wa kiapo ambao uligawanyika katika sehemu tatu na kila alipomaliza sehemu moja alisema, “Ee Mwenyenzi Mungu nisaidie” na mara zote alikuwa akishangiliwa.

Alianza kusoma kipengele cha kwanza cha kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikafuatiwa na kipengele cha kufanya kazi bila upendeleo na kuzingatia sheria, akamalizia na kipengele cha kutunza siri ya Baraza la Mawaziri.

Baada ya kumaliza kula kiapo  lilifuatia tukio la viongozi kutoa mkono wa pongezi kwa Waziri Mkuu huyo mpya ambapo waliitwa kwa majina mmoja mmoja na kwenda kumshika mkono.

Rais Magufuli ndiye aliyeanza kumpa mkono wa pongezi akifuatiwa na Makamu wake, Samia Hassan Suluhu; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Idi; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na Pandu Amir Kificho, Spika wa Bunge la SMZ na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande.

Wengine waliompa mkono wa pongezi ni Jaji Mkuu wa SMZ, Omar Othman Makungu; Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Abdulhamid Yahya Mzee akafuatiwa na mke wa Majaliwa, Mary Majaliwa na baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, George Masaju.

Makamu wa Rais mstaafu, Mohamed Gharib Bilal, aliliwakilisha kundi la viongozi wastaafu kutoa mkono wa pongezi kwa Waziri Mkuu Majaliwa.

Pia viongozi hao wote pamoja na ndugu wa Waziri Mkuu walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na baadaye wakaendelea na shamrashamra zilizopambwa na ngoma kabla ya kuelekea bungeni kusikiliza hotuba ya uzinduzi wa Bunge ya Rais Magufuli.

 

MAALIM SEIF, LOWASSA, SUMAYE WASUSA TENA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameendelea kutohudhuria sherehe za kuapishwa viongozi wa juu wa serikali ya awamu ya tano tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania bara na kufutwa kwa matokeo yote ya Uchaguzi wa Zanzibar.

Maalim Seif, ambaye hakuonekana jana wakati Majaliwa akiapishwa, hii ni mara ya pili kwake kutohudhuria sherehe kama hizo ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni wakati Rais John Magufuli akiapishwa Novemba 5, mwaka huu, baada ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza kususia sherehe hizo.

Msimamo huo wa Ukawa ulitokana na kile walichodai ni kutoridhishwa kwao na mchakato wa uchaguzi, hususan matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, yakishatangazwa hakuna haki ya kuyapinga katika mahakama yoyote.

Viongozi wengine ambao nao walitakiwa kushiriki katika sherehe hizo na ambao hawakuhudhuria zote ni Mawaziri Wakuu wastaafu, Federick Sumaye na Edward Lowassa, ambao wote walikihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia upinzani wakiiunga mkono Ukawa.

Sababu nyingine zilizotajwa za viongozi hao kutohudhuria matukio hayo makubwa ya kitaifa ni kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichodai ni kuwepo kwa kasoro nyingi katika uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles