Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa msaada wa Sh milioni 10 kumuwezesha Ernest Masenga kutatua changamoto zinazomkabili.
Masenga alikuwa msanii wa muziki wa dansi na hivi sasa anasumbuliwa na maradhi ya miguu. Pia makazi anayoishi si salama na yanahitaji kukarabatiwa.
Majaliwa alitoa msaada huo Dares Salaam jana baada ya kuguswa na hali ya maisha ya msanii huyo aliyemuona kupitia kipindi maalumu kilichoonyeshwa na TBC Sepemba 5, mwaka huu. Kipindi hicho kiliongozwa na Godfrey Nago.
“Nawaomba Watanzania wenzangu tumsaidie mwezetu aweze kuishi vizuri kwa sababu sanaa yake imesaidia kuelimisha na kuburudisha umma,” alisema Majaliwa
Nago ambaye alipokea msaada huo kwa niaba ya Masenga, alisema atahakikisha anasimamia vizuri fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa.
Alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuwaunga mkono na kutoa msaada huo kwa sababu ameonyesha Serikali inawajali wananchi wake na TBC itaendelea kuwaomba wadau mbalimbali wajitokeze kumsaidia msanii huyo.
Mjomba wa msanii huyo, Kanuti Mloka ambaye aliiwakilisha familia, alimshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo.
Alisema familia imeshindwa kumsaidia Masenga kutokana na hali duni ya maisha waliyonayo.