26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mhagama aridhishwa na utendaji TACAIDS

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI zimeendelea kuimarika hapa nchini.

Mhagama ameyasema hayo Februari 4, 2021katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za ulevya iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ikilenga kujenga uwezo kwa wajumbe hao kuhusu majukumu ya Tume na utekelezaji wake.

“Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI milioni 1.2 walikuwa wanapata huduma za dawa za kufubaza virusi hivyo pamoja na kuimarika kwa huduma za upimaji wa virusi hivyo na utoaji wa elimu kuhusu Virusi hivyo na UKIMWI,” alisema Mhagama.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akieleza jambo kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati Februari 4, 2021 bungeni jijini Dodoma.

Aliongeza kuwa, ofisi yake kupitia Tume ya Kuthibiti UKIMWI nchini itaendelea kutoa elimu kuhusu kinga dhidi ya VVU ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU hususani kwa vijana kupitia kampeni mbalimbali za mabadiliko ya tabia zinazolenga kuyafikia makundi yote.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Alice Kaijage, amesema kuwa wajumbe wa Kamati hiyo wataendelea kutoa michango yao ili kuiwezesha Tume hiyo kuimarisha zaidi utendaji wake hasa katika mapambanao dhidi ya UKIMWI.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga akisisitiza kuhusu Ofisi hiyo kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo bungeni jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe.Ummy Nderiananga amesema kuwa Ofisi hiyo itachukua na kufanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo ili kuimarisha utendaji wa Tume na Mapambano dhidi ya UKIMWI.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo, Dk. Leonard Maboko amesema kuwa kwa sasa mwamko wa wananchi kujitokeza kupima na kujua hali zao umeongezeka katika makundi mengi isipokuwa kundi la wanaume bado mwamko hauridhishi.

“Inakadiriwa hadi kufikia Desemba 2019 watu wazima 1,612,301 wenye miaka 15 na zaidi walikuwa wameambukizwa Virusi vya UKIMWI ambapo wanawake ni 983,471 na wanaume 628,830 na watoto chini ya miaka 15 walikuwa 93,000,”alieleza Dk. Maboko.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya, Dk. Alice Karungi Kaijage akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa Semina kwa wajumbe hao iliyoandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo aliipongeza Tume kwa kuwajengea uwezo kuhusu muundo na utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha alitoa rai kwa kundi la vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi kupima na kujua hali zao.

“Kamati tumefarijika kwa namna Tume ilivyojipanga kuhakikisha inaendelea kuelimisha makundi yanayoongoza kwa maambukizi mapya hasa vijana hivyo ni vyema kundi hili likawekewa mikakati ya makusudi ili kusaidia kukabili hali hiyo, kamati itaendelea kuunga mkono mapambano hayo,” amesema.

Sehemu ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya wakifuatilia uwasilishwaji wa mada kuhusu masuala ya UKIMWI iliyolenga kuwajengea uwezo iliyandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania jana Februari 4, 2021 bungeni jijini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles