26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MASAUNI AWEKA KITIMOTO JESHI LA POLISI

Na ELIUD NGONDO, MBEYA


Hamadi MasauniNAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni ameliweka kitimoto Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana .

Kutokana na hali hiyo, Waziri Masauni ametoa wiki moja kwa jeshi hilo kuwakamata wauzaji.

Naibu waziri Masauni, alitoa agizo hilo juzi mkoani Mbeya alipokuwa katika ziara ya kutembelea idara mbalimbali za Serikali zilizo chini ya wizara yake ambazo ni jeshi la polisi, jeshi la magereza, jeshi la Zimamoto na Idara ya Uhamiaji.

Alisema takwimu zinaonyesha Mkoa wa Mbeya,kuna ongezeko kubwa la matumizi ya dawa za kulevya, lakini  jeshi  hilo halijaonyesha jitihada za maksudi kukomesha mnyororo wa uuzwaji wa dawa hizo.

Alisema kama watumiaji wa dawa hizo wanafahamika, vilevile ni rahisi kuwatambua wauzaji kwa kuwabana hao hao watumiaji ili wawataje  wanaowauzia.

“Haiwezekani watumiaji wa unga wanafahamika lakini wanaowauzia wasifahamike, pia hatuwezi kuvumilia vijana wetu ambao ndio nguvukazi ya taifa wakaendelea kuharibika, sasa nawapa wiki moja kuhakikisha mnaubaini mtandao wanaouza dawa hizo na kuwachukulia hatua,” aliagiza Masauni.

“Kamateni mateja ili wawaonyeshe wanakonunua ‘unga’ huo, hapo  mtakapoweza kuvunja mnyororo wa biashara hiyo na kuwaokoa vijana wetu,” alisisitiza.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, alikiri kuongezeka kwa matumizi ya dawa hizo,akasisitiza  tayari wameshaanza kuchukua hatua za kuuvunja mtandao wa wauzaji kwa kuwakamata watumiaji.

Alisema  ndani ya siku tatu zilizopita walifanya operesheni ya kuwasaka na kuwakamata baadhi ya ‘mateja’ ambao nao wameshawataja wanaowauzia lakini akaeleza kuwa changamoto iliyojitokeza ni wauzaji hao kukimbilia mikoa ya jirani na nchi jirani.

Aliziitaja changamoto nyingine kuwa ni makampuni ya simu kutotoa ushirikiano kwa Jeshi hilo katika kuwafuatilia wahusika wa kuuza dawa hizo walipo.

“Jana (juzi) tulifanya operesheni na tulifanikiwa kuwakamata baadhi ya watumiaji ambao tumeshawafungulia kesi na wametutajia majina na namba za wanaowauzia, lakini hao wauzaji baada ya kupata taarifa wamekimbilia mikoa inayotuzunguka na nchi jirani za Zambia na Malawi,” alisema Kuzaga na kuongeza.

“Kutokana na watumiaji kutupatia namba za Simu za wanaowauzia, tuanajaribu kuyatumia makampuni ya simu husika ili ‘kuwatrace’ yaani kuwafuatilia ili tutambue walipo, lakini wenzetu wa mitandao husika hawatupatii ushirikiano,” alisema Naibu.

Katika hatua nyingine, Waziri Masauni aliliagiza Idara Uhamiaji kuongeza jitihada katika kuwakamata wahamiaji haramu pamoja na watu wanaowasafirisha kisha kuwachukulia hatua.

Alisema kwa jiografia ya Tanzania, Mkoa wa Mbeya ndilo lango kuu la wahamiaji kutoka nchi za Somalia, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi zingine kutoka na kuingia nchi jirani ya Malawi kuelekea kusini.

Aliliagiza Jeshi hilo kuwathibiti wahamiaji hao pamoja na wale wanaowasafirisha na kwamba lengo la Serikali ni kutaka kuutumia Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kukomesha mtandao huo.

Alisema wasafirishaji wa wahamiaji hao kutoka mikoa mingine kupitia Mbeya yawezekana ni wenyeji wa Mbeya au ni wazoefu na mkoa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles