23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

‘WANAWAKE WENGI HAWANUFAIKI NA KILIMO’

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


kilimoLICHA ya wanawake kutumia muda wao mwingi katika shughuli za kilimo, hata hivyo wengi hawanufaiki kabisa na jasho la kazi zao.

Hali hiyo inasababishwa na kuwapo kwa tamaduni na mila zisizozingatia usawa wa kijinsia na unyanyasaji, kutopewa haki sawa ya kumiliki ardhi na uwepo wa sheria kandamizi.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa mradi wa ubunifu katika masuala ya kijinsia kuimarisha uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya wa Shirika la Land O’Lakes, Dk. Rose Kingamkono, alisema katika maeneo mengi wanawake ndio wamekuwa wahusika wakuu wa kilimo.

“Katika maeneo mengi nchini, wanawake ndio ambao wanahusika katika hatua zote za awali za kilimo ambazo ni uandaaji wa shamba, upandaji wa mazao, upaliliaji wa shamba, utunzaji, uvunaji, uhifadhi na usindikaji.

“Lakini wanaume wao huusika katika hatua za mwishoni pekee hasa uuzwaji wa mazao na maamuzi kwenye matumizi ya mapato ambayo yanatokana na jasho la mwanamke,” alisema.

Alisema baadhi ya sheria zilizopo ikiwamo ile ya kimila zinapaswa kuangaliwa upya ili kukabili hali hiyo.

“Kwa sababu kuendelea kufumbia macho hali hii huleta shida mbalimbali si tu kwa wanawake bali familia na jamii kwa ujumla, hakuna usawa wa kijinsia, wanawake wanatumia muda mwingi kuzalisha, lakini hawafaidiki kwa jasho lao na mchango wao hautambuliki,” alisema.

Dk. Kingamkono alisema kwa kuwa wanawake hukosa udhibiti wa maamuzi ya fedha zitokanazo na kilimo hushindwa kufanya maamuzi ya kununua dhana bora za kilimo.

Naye mtaalamu mwelekezi kwenye masuala ya jinsia na utawala bora katika shirika hilo, Magreth Henjewele, alisema tafiti nyingi zinaonesha wanawake wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula, hata hivyo bado sheria haziwapi kipaumbele.

“Utafiti wa masuala ya kazi na ajira wa 2014 uliofanyika nchini unaonesha wanawake wanachangia asilimia 60 katika uzalishaji wa chakula lakini wanaohusika katika uuzaji ni wanaume.

“Mila na desturi zinatoa majukumu machache kwa wanaume lakini ndilo kundi kubwa linalonufaika wakati wanawake wakipewa majukumu makubwa na wananufaika kidogo,” alisema.

Alisema shirika hilo limedhamiria kupeleka elimu kwa jamii kuhusu masuala hayo na kwamba tayari wamefikia mikoa mitatu ambayo ni Iringa, Morogoro na Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles