Mwandishi Wetu-Liwale
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametatua mgogoro uliodumu kwa miaka 12,kati ya pori la akiba la Selous na wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu kilichopo Wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
Mgogoro huo, ulianza mwaka 2007,baada ya wananchi kuanza kudai kuwa eneo la Kihulumira ambalo linapakana na pori la akiba la Selous kuwa ni moja ya maeneo yao ya asili.
Kutokana na hali hiyo, kulisababisha uhasama mara kwa mara, kati ya wananchi na askari wanyamapori, hasa pale wananchi walipokuwa wakikamatwa kwa madai wameingia ndani ya hifadhi bila kibali.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu,baada ya kutembelea eneo hilo juzi, Waziri Kanyasu alisema lilisajiriwa mwaka 1975, huku kijiji kikisajiliwa mwaka 2005.
Alisema baada ya kuundwa timu hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilibainika eneo hilo si la wananchi na wala sio sehemu ya pori la akiba la Selous, bali ni pori tengefu ambalo ni mali ya Serikali Kuu na linasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika hatua nyingine, Waziri Kanyasu aliwataka wananchi kuacha vitendo vya kukata miti na kuchoma misitu kutokana na uharibifu mkubwa wa misitu aliuona karibu na eneo hilo.
Aliwaagiza viongozi wa vijiji kuweka sheria kali ili kudhibiti hali ya uharibifu wa misitu,unaoendelea katika maeneo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wanachi wa Wilaya ya Liwale, Mbunge Liwale, Zuberi Kuchauka alishukuru Serikali kwa hatua iliyofikia,mgogoro huo, ni wa muda mrefu na ulikuwa haujapatiwa ufumbuzi.
Alisema mgogoro huo, uliwafanya wananchi wa maeneo hayo kupunguza kasi ya kujiletea maendeleo,badala yake wajanja wachache waliokuwa wakitumia nafasi ya mgogoro kuendelea kujinufaisha.
” Sitegemei mgogoro mwingine wa ardhi,baada ya kumalizika huu, nawaomba wananchi sasa tuchape kazi,”alisema Kuchauka.
Kutokana na kumalizika kwa mgogoro huo, wananchi wa kijiji hicho, wameiomba Serikali kulitumia eneo hilo kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA) ili kuinua kipato katika kijiji hicho.