24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

UTEUZI WA KASEJA NI KIELELEZO CHA UDHAIFU WA SOKA LETU?

SOSTHENES NYONI

KAMA kuna mchezaji anayepaswa kuwa mfano wa kuigwa na wengine ndani ya kipindi cha miaka zaidi ya kumi na tano iliyopita, basi ni mlinda mlango Juma Kaseja.

Kaseja ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 34, ana sifa zote anazopaswa kuwa nazo mchezaji anayejitambua, hizi ni pamoja na kujituma na nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Ni kutokana na sifa hizo, Kaseja ameendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa hapa nchini, licha ya kwamba mpaka sasa ameutumikia mchezo wa soka katika ngazi ya ushindani karibu miaka 20.

Ukubwa wa jina lake hautoni na matukio ya utovu wa nidhamu, isipokuwa uwezo wake mkubwa wa kusimama langoni na kujiheshimu akitambua soka ni kazi kama  zilivyo kazi nyingine.

Kwakukumbukusha tu ni kwamba, Kaseja ninayemzungumzia hapa ni yule aliyeiongoza Simba kuwatupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, waliokuwa mabingwa watetezi, timu ya Zamalek ya Misri, mwaka 2003.

Kaseja aliivusha Simba, baada ya kupangua mikwaju miwili ya penalti na kuwafanya Wekundu hao kuibuka na ushindi wa penalti 2-1.

Pia ametwaa mataji mengi ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Simba aliyoichezea kwa misimu mingi, baada ya kumsajili akitokea Moro United.

Baada ya kuitumikia Simba kwa muda mrefu, mwaka 2013 alijiunga na Yanga,ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Mbali ya kuzichezea Simba na Yanga kwa mafanikio makubwa, pia amepata kuzichezea Mbeya City, msimu wa 2015-16, Kagera Sugar 2016-18, kabla ya msimu uliopita kujiunga na timu ya KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambayo msimu uliopita aliisaidia kumaliza Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya nne.

Nafasi hiyo imeiwezesha KMC kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Azam FC, huku Simba na Yanga zikikata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kaseja ameichezea timu za Taifa ya Tanzania za umri tofauti kwa vipindi tofauti.

Alianza kuichezea timu ya taifa, mwaka 2001 na kudumu nayo hadi mwaka 2007.

Baada ya hapo, alikuwa nje ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’, kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi  hadi mwaka 2009, aliporejeshwa kikosini.

Tangu wakati huo amekuwa akiingia na kutoka katika kikosi cha Taifa.

Kaseja hivi karibuni aliteuliwa katika kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya michezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan).

Taifa Stars ilipangwa kuanza kampeni zake kwa kuumana na Kenya (Harambee Stars), mchezo wa kwanza ulichezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa suluhu.

Mchezo wa marudiano ulitarajiwa kuchezwa jana jioni, Uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi, Kenya.
Tangu mwaka 2003, hadi leo imepita miaka 16, lakini mlinda mlango huyu ameendelea kudaka katika kiwango cha juu.

Hata hivyo, pamoja na kudumu katika kiwango bora kwa kipindi chote hicho, kuondoka kwake Simba kwenda Yanga wakati huo kulihusishwa na kushukwa kiwango, jambo ambalo kiuhalisia halikuwa na ukweli wowote.

Lakini kitendo cha kuachwa katika kikosi cha Taifa Stars, kilikuwa mwendelezo wa tabia iliyojengeka miongoni mwa wadau wa soka hapa nchini, kwamba mchezaji akicheza kwa muda mrefu basi ni mzee.

Tabia au utamaduni huu umekuwa ukiwathiri wachezaji wengi wa Tanzania, kwakua hujikuta wakitundika daruga kwa hiyari au lazima, licha ya ukweli kwamba bado walikuwa na nguvu za kuzitumikia klabu zao au timu ya taifa.

Je, Ndayiragije ametuumbua?

Hatua ya kocha wa muda wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije kumjumuisha katika kikosi kinachosaka tiketi ya Chan ni ushahidi mwingine kwamba kuna mahali hatuwatendei haki wachezaji wetu.

Kaseja yule yule aliyeonekana ni mzigo Simba miaka mitano nyuma, ndiye huyu huyu aliyeaminiwa na Mrundi Ndayiragije na kuiongoza Stars kutoka suluhu na Kenya katika mchezo wa kwanza.

Pia ndiye aliyeiongoza KMC kumaliza nafasi ya nne msimu uliopita na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho.

Ndayiragije ametuonyesha kwamba, kuna wakati tunapaswa kuacha kuendesha soka kwa mihemuko na ushabiki usiokua na tija.

Ni wazi kuna kitu cha kipekee katika mikono ya Kaseja, ambacho Ndayiragije amekiona na ndio maana hakusita kupendekeza kwa uongozi wa KMC umpe mkataba wa miaka mitatu, baada ya ule wa awali kumalizika msimu wa Ligi Kuu uliopita ulipofikia tamati.

Tumeshuhudia sajili zilizofanywa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu, kwa ajili ya msimu ujao, wachezaji wengi wakiingia mikataba ya chini ya miaka miwili ikiwemo pale KMC, lakini kitendo cha Kaseja kuongeza miaka mitatu kinathibitisha ubora wake na kufuta dhana kwamba ni mzee na hana jipya tena katika soka la ushindani.

Kaseja ataondoka uwanjani kama ilivyo kwa wafanyakazi wa taaluma nyingine yoyote ile, lakini ni bora tukamwondoa yeye na wengine kwa vigezo vya msingi, ambavyo ni pamoja na uwezo mdogo langoni na nidhamu.

Kaseja anaweza kuwa mwalimu mzuri kwa wachezaji wengine wenye ndoto kama yake ya kudumu katika soka wakiwa kwenye kiwango cha juu.

Tumemshuhudia kipa wa kimataifa wa Uganda na klabu ya Mamelod Sundown, Denis Onyango akiendelea kutoa mchango mkubwa katika soka.

Tulimwona alivyosimama vyema katika lango la Uganda, na kuisaidia kufuzu robo fainali  ya Kombe la Mataifa ya Afrika(Afcon), zilizofanyika nchini Misri, kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles