26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI: KANUNI SHERIA YA HABARI ZIMEKAMILIKA

Na MAREGESI PAUL, DODOMA

SERIKALI imekamilisha kutunga kanuni za Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016.

Taarifa hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

“Nimewaita hapa leo (jana) kwa lengo la kuwapa taarifa rasmi wana taaluma ya habari na wananchi kwa ujumla kuhusu Sheria ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 65 cha sheria hiyo, nikiwa kama waziri wa habari, nimepewa jukumu la kutunga kanuni za kusaidia utekelezaji wa sheria hii.

“Napenda kuwashukuru wadau wengi walioleta maoni yao tena kwa kujenga hoja kwa maandishi na utafiti na ninayo furaha leo kuwataarifu kuwa, tumefaidika sana juu ya maoni hayo na kanuni hizo sasa zimeshachapishwa kwenye Gazeti la Serikali la Februari 3, 2017.

“Kanuni hizi, zimesheheni masuala ya kusaidia utekelezaji wa sheria na hasa muktadha mzima wa kuifanya Tanzania kuwa na kile nilichokiainisha juu ya vyombo vya habari vyenye uhuru wa kutosha.

“Tulisoma na kuchambua maoni ya wengi juu ya kiwango cha elimu anachotakiwa kuwa nacho mwandishi wa habari kwani baadhi walitaka iwe ni cheti, wengine iwe ni diploma, wengine walitaka iwe ni degree, wengine walitaka iwe ni PhD na wengine walitaka awe ni mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika.

“Katika mjadala huo, Serikali ilisimama katikati na kuamua kwamba, sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni diploma ya uandishi wa habari.

“Hata hivyo, Serikali imetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kuanzia Januari mosi, mwaka huu kwa waandishi waliopo sasa na wanaotaka kuingia katika taaluma hii ambao hawana sifa hizi, wakasome ili wawe na sifa.

“Ili kuwasaidia wana habari hasa waliopo sasa kazini waweze kujiendeleza, kupitia Idara ya Habari (Maelezo), tutaendelea kutoa press card bila kuwabana sana waandishi wa habari kwa kuangalia vigezo hivi vya kitaaluma, bali dhamana ya waajiri wao,” alisema Nape.

Wakati huo huo, Nape alilipongeza Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwa kile alichosema lilichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa kanuni nzuri za sheria hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles