29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Jenista aitaka TACAIDS kukabili maambukizi mapya

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ameitaka Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi, (TACAIDS) kusimamia mikakati ya kukabili maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa huo.

Waziri Mhagama amesema hayo leo Agosti 10, 2021, wakati akizindua Kamisheni ya TACAIDS, akitaja  maeneo yanayohitaji jitihada hasa vijana ambao wanatajwa kuwa hatarini kupata maambukizi.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni  kuhamasisha upimaji kwa wanaume na watoto,kuimarisha huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kuondoa ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU.

“Kuna maeneo mengine ambayo kamisheni inatakiwa kufuatilia kwa ukaribu  matumizi ya rasilimali fedha na watu ndani ya tume na mfuko wa Ukimwi pamoja na mkakati wa usambazaji wa kinga na tathimini ya mkakati wa Dunia unaokwisha na ujao wa ndani,” amesema Jenista.

Akizungumzia hali ya maambukizi nchini amesema, takwimu zinaonyesha Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano ya VVU kwani kiwango cha upimaji wa afya kimeongezeka kutoka asilimia 61 kwa mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 mwaka 2019.

“Matumizi ya dawa za kufubaza VVU yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi asilimia 98 mwaka 2019, vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka 64,000mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020 na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kwa asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020,” ameeleza.

Kwa upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga alihimiza ushirikishwaji wa kundi la watu wenye ulemavu katika kamisheni hiyo kurahisisha kufikisha mapendekezo na ushauri kulinda na kusimamia haki za watu wenye ulemavu wanaoishi na virusi na ambao hawajapata maambukizi.

“Katika vita hivi hatuwezi kuliacha kundi la wenye ulemavu, tunatambua wapo wanaoishi na maambukizi na wengine hawana hivyo uwepo wa mwakilishi angalau mmoja katika kamisheni hii itakuwa msaada mkubwa watafikiwa kwa urahisi,” amefafanua Ummy.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya TACAIDS,Tanzania Dk. Hedwiga Swai, amebainisha kwamba kufanikisha vita dhidi ya Ukimwi inahitaji ushirikiano wa taasisi zote, taasisi za dini na kila mmoja kwa nafasi yake kufikia malengo ya kimataifa ifikapo 2030 kutokomea maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na Ukimwi na unyanyapaaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles