Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Ununuzi wa Mahindi cha Kizuka, mkoani Ruvuma, Septemba 18, 2024, ambapo alikutana na wakulima waliokuwa wakichekecha na kuchambua mahindi. Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Bashe alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kutatua changamoto za wakulima kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Baadhi ya wakulima waliopata nafasi ya kueleza changamoto zao ni Nicodem Mayo, Zena Zawamba, Paul Philemon Haule, na Baltazari Komba Mjinga. Wakulima hawa walieleza kuwa wamevuna zaidi ya magunia 330 kutoka kwenye mashamba ya hekari 15.
Hata hivyo, waliomba mawakala wanunue mahindi kwa bei ya shilingi 600 hadi 650 kwa kilo badala ya sh350, ambayo imekuwa ya hasara kwao. Pia walihitaji miundombinu bora ya barabara, mashine za kisasa za kuchambua mahindi, zana bora za kilimo, mbegu za kisasa, na huduma za maafisa ugani.
Waziri Bashe, akijibu hoja hizo, alieleza kuwa serikali imeona uhitaji wa kuboresha huduma kwa wakulima kupitia uwekezaji wa mashine za kisasa. “Nimeelekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mashine za kisasa za kuchambua na kusafisha mahindi ili kurahisisha kazi kwa wakulima,” alisema Waziri Bashe.
Aidha, alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Wilman Kapenjama Ndile, kuhakikisha mawakala wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wananunua mahindi kutoka kwa wakulima kwa shilingi 700 kwa kilo, na kama hilo haliwezekani, wafanye ununuzi wa moja kwa moja kupitia NFRA.
Kwa upande mwingine, wakulima hao walipata ahadi ya kuongezewa maghala ya kuhifadhi mazao, kupatiwa mizani za kisasa za kidigitali, na kujengewa Kituo cha Zana za Kilimo. Pia, waliahidiwa mbegu za ruzuku, zikiwemo aina za Hybrid na OPV, pamoja na mbolea za ruzuku.
Kuhusu miundombinu ya barabara na mawasiliano, Waziri Bashe aliahidi kushirikiana na viongozi wa sekta husika ili kuboresha hali hiyo kwa manufaa ya wakulima.
Katika ziara hiyo, Waziri Bashe pia alitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ambapo alikubali ombi la Mkuu wa Mkoa kutumia shamba la tumbaku la Ruvuma kuwa shamba la BBT kwa matumizi ya wakulima wa eneo hilo.