24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Aweso kuja na mageuzi makubwa sekta ya maji

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali inataka kufanya mageuzi makubwa katika mamlaka zote nchini kwa sababu kuna maeneo mengine watu wamejisahau.

Ameyasema hayo leo Desemba 23 wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa maji wa Kisarawe – Pugu – Gongo la mboto.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, akifunga mita kuashiria kuanza kwa huduma ya maji kwa wananchi wa Kifuru alipotembelea mradi wa maji Pugu.

Amewataka wataalam wa wizara ya maji na mamlaka zote za maji kuacha kufanya kazi kwa mazoeya badala yake watatue kero za wananchi.

“Tusizoee shida za wananchi, si vema hata kidogo au ijengeke tabia kuona mwananchi wa kijijini kunywa maji na punda au kunywa maji na mifugo ikawa ni haki yake. Isijengeke tabia kujitafunia kijanja kijanja fedha za miradi, niwaambie wazi hatuwezi kuvumilia mambo ya namna hiyo tunataka wahandisi wote wa maji twendeni tukatatue tatizo la maji na si blaa blaa,” amesema Aweso.

Waziri huyo pia ameipongeza Dawasa kwa kutekeleza agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli la kufikisha huduma ya maji katika majimbo ya Ukonga na Segerea kabla ya Desemba 25 na kuitaka iongeze kasi ya kuwasambazia wananchi.

Mradi huo utahudumia wakazi wa Jimbo la Ukonga ikiwemo Pugu, Majohe, Gongo la mboto, Bangulo, Airwing, Kigogo, Chanika, Kinyamwezi, Banana, Segerea na Kifuru.

Tanki hilo linalopokea maji kutoka Kisarawe kwenda Pugu lenye uwezo wa kusambaza lita milioni 2.8 kwa siku limegharimu Sh bilioni 6.9.

Naye Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyrpian Luhemeja, amesema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo kutawezesha wananchi wa majimbo ya Ukonga na Segerea kupata maji ya uhakika.

“Tumekamilisha mradi kwa awamu ya kwanza, tumeingiza maji kwenye tanki, tumekamilisha kulaza mabomba kilomita 13.5 kutoka Kisarawe na kilomita 28 kuelekea Chanika, hiyo ni kiashiria kwamba maji jimbo la Ukonga sasa yanapatikana.

“Sasa tunaanza safari ya kwenda Kinyerezi, Kifuru, Segerea na Tabata wananchi wajitokeze kuunganishiwa maji,” amesema Luhemeja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, amewataka wakazi wa jiji hilo kulipa bili kwa wakati na kulinda miundombinu ya maji.

“Tunapoona watu wanaiba maji au kufanya uharibifu wa miundombinu tuwe waungwana tutoe taarifa na tuchukue hatua. Tuache polisi wafanye kazi zingine sisi wenyewe tulinde miundombinu,” amesema Kunenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles