26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri atoa wiki kiwanda kuboresha mazingira ya kazi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, ametoa wiki mbili kwa uongozi wa kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kilichoko Kigamboni Dar es Salaam kuboresha mazingira ya kazi ambayo yameonekana kuhatarisha afya na usalama wa wafanyakazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha matokeo ya ukaguzi wa masuala ya usalama na afya katika Kampuni ya Lake Oil Group Kigamboni mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, wakati wa ziara iliyolenga kufuatilia uzingatiaji wa Sheria za Kazi katika maeneo ya kazi Kigamboni, Dar es Salaam.

Maagizo hayo yametolewa kufuatia makubaliano baina ya uongozi wa kiwanda na Waziri alipotembelea kiwanda hicho Oktoba 27, 2022 akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda na watendaji wengine wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Mwenye kiwanda asitishe kwanza shughuli hasa kwenye maeneo yale yanayozalisha maji machafu na maeneo mengine ambayo tumekuta yana mpangilio mbaya wa malighafi na vifaa vya kufanyia kazi ili aweke mazingira vizuri. Tumekubaliana nae kufanya hivyo na ahakikishe kwamba katika kipindi hicho anachofanya maboresho wafanyakazi wanashiriki shughuli hiyo na awalipe stahiki zao kama kawaida.

“Tunawapenda sana wawekezaji wetu kwakuwa wanatusaidia kutengeneza ajira za Watanzania lakini tunawaomba wajitahidi kuzingatia sheria za nchi ikiwemo kuweka mazingira ya uzalishaji katika hali nzuri ili kuwaepusha wafanyakazi na magonjwa na ajali zinazoweza kusababishwa na mazingira ya kazi yasiyokuwa rafiki,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (aliyevaa koti la bluu) akipokea maelezo kutoka kwa mwakilishi wa Kampuni ya Lake Oil Group kuhusu shughuli zinazotekelezwa na kampuni hiyo. Alioambatana nao ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa (kulia kwa Waziri), Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (kulia kwa Mkuu wa Wilaya) na Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa (kushoto kwa Waziri).

Awali, akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa, amesisitiza kuwa kazi hiyo ya maboresho ifanyike kwa kuwatumia wafanyakazi wa kiwanda hicho na kusimamiwa na watendaji wa Ofisi yake pamoja na wale wanaotoka katika Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wenye viwanda kuwajali wafanyakazi ambao ndio msingi mkubwa wa uzalishaji kwa kuwapa vifaa kinga stahiki pamoja na mahitaji mengine ya muhimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akiwa katika kikao na wawakilishi wa uongozi wa Kampuni ya Lake Oil Group (hawapo pichani) wakati wa ziara iliyolenga kufuatilia uzingatiaji wa sheria mbalimbali za kazi katika maeneo ya kazi Kigamboni, Dar es Salaam. Alioambatana nao ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa (Kushoto) na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (kulia).

“Katika ukaguzi wetu tumebaini kwamba baadhi tu ya wafanyakazi ndio wanaopatiwa vifaa kinga na wengine hawapewi. Aidha, wafanyakazi hawapatiwi maji safi na salama ya kunywa kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi jambo ambalo ni muhimu sana hususan kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye maeneo yenye joto kali. Hata hivyo pamoja na kwamba suala hili lipo kisheria lakini ni jambo la kiutu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA katika kikao cha pamoja baada ya ukaguzi katika kampuni ya Lake Oil Group.

Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda hicho, Zhang Ping, ameahidi kufanya maboresho yaliyopendekezwa na wataalam ndani ya muda uliokubaliwa na pande zote mbili.

Aidha, ujumbe huo wa Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi umetembelea Kampuni ya Lake Oil Group na kufanya ukaguzi wa mazingira ya kazi pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni hiyo.

Ziara hii ni sehemu ya ziara ambazo Waziri huyo amekuwa akizifanya katika mikoa mbali mbali kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Sheria za Kazi yakiwemo Masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi, Hifadhi kwa Jamii na Mahusiano Kazini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo changamoto wanazokumbana nazo katika shuguli zao za uzalishaji katika kiwanda hicho.

Kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kinazalisha bidhaa mbali mbali za plastiki yakiwemo mabomba ya maji na vyombo vya majumbani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (aliyevaa koti la bluu), akiwasikiliza Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda na Meneja wa OSHA Kanda ya Pwani, George Chali, wakati wa ziara iliyolenga kufuatilia uzingatiaji wa sheria mbalimbali za kazi katika maeneo ya kazi Kigamboni, Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (mwenye koti la bluu) akiwasikiliza wafanyakazi wa Kampuni ya Lake Oil Group alipokuwa akifanya ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria za Kazi katika maeneo ya kazi Wilaya ya Kigamboni ikiwemo Kampuni hiyo.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles