28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu 1,952 wafunguliwa mashtaka TSC

*Ni katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo 919 wamefukuzwa kwa utoro, ulevi…

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Katika kipindi cha machi mwaka jana hadi Septemba mwaka huu Walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu ambapo kati yao 919 walifukuzwa kazi kutokana na utoro, ulevi,kugushi vyeti na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.

Hayo yameelezwa Oktoba 27, jijini Dodoma na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama wakati akiwasilisha mbele ya waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za tume hiyo kwa mwaka 2022-2023.

Nkwama amesema pamoja na jitihada za kutoa elimu bado kuna walimu ambao wamekuwa hawazingatii miiko na maadili ya kazi yao.

Amesema walimu wenye tabia hizo hufikishwa katika mamlaka  za kinidhamu kwa ajili ya kushughulikiwa kwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili kuwanusuru watoto kupata huduma ya elimu isiyokusudiwa na Taifa.

Amesema katika kipindi cha Machi mwaka jana hadi Septemba mwaka huu walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu katika mashauri hayo 1,362 sawa na asilimia 69.8 ya mashauri yote yalihusu utoro.

“Kuna mashauri 260 sawa na asilimia 13.3 ya mashauri yote yalihusu kughushi vyeti, 119 yalihusu mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, 98 yalihusu ukaidi, 66 sawa na asilimia 3.4 yalihusu ulevi, 16 sawa na asilimia 0.8 yalihusu ubadhirifu na mashauri 31 sawa na asilimia 1.6 yalihusu makosa mengineyo.

“Mashauri 1,642 yaliyoamuliwa walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, walimu 115 sawa na asilimia saba ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo,”amesema Katibu huyo.

Amesema  walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu, walimu 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio.

“Walimu 59 sawa na asilimia 3.6 walipewa adhabu ya onyo na walimu 77 sawa na asilimia 4.7 walipewa adhabu ya kufidia hasara,” amesema.

Amesema TSC makao makuu ilipokea nakala ya rufaa 64 zilizokatwa kwa rais kupinga uamuzi wa tume.

“Tuliandaa mwenendo na vielelezo vya rufaa 56 na kuwasilisha kwa rais ambapo tume inaendelea kuandaa mwenendo na uchambuzi wa rufaa 8 zilizobaki kwa hatua ya kuwasilishwa,”amesema Katibu huyo.

Akitaja mafanikio iliyopata tume katika uongozi wa serikali ya awamu ya sita Katibu huyo amesema walimu 16,749 waliajiriwa, wakiwemo 8,949 wa shule za msingi na 7,800 wa shule za sekondari.

Amesema walimu 15,802 walisajiliwa ambapo kati yao  walimu wa shule za msingi walikuwa 8,512 na Sekondari walikuwa 7,290.

Amesema walimu 6,949 sawa na asilimia 100 walithibitishwa kazini wakiwemo 3,949 wa Shule za Msingi na 3,000 wa shule za sekondari.

Kuhusu walimu kupandishwa madaraja Katibu huyo amesema katika kipindi cha nyuma kilio kikubwa cha walimu kilikuwa ni kucheleleweshwa kupanda vyeo.

Amesema zoezi hilo hufanywa kwa kushirikiana na waajiri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Katibu huyo amesema walimu 47,158 walipandishwa vyeo kati yao 22,943 ni wa shule za msingi na 11,524 wa sekondari kwa mwaka huu wa fedha huku walimu 12,546 walibadilishiwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles