31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAZAZI WATOTO WALIOTEKWA, WAZUNGUMZIA UCHUNGUZI

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

WAZAZI wa watoto Maureen David (6) na Ikram Salim (3), waliotekwa na kukutwa wakiwa wamefariki katika shimo la maji taka eneo la Uzunguni, Mtaa wa Olkerian Kata ya Olasiti, wameeleza kile walichokishuhudia kwenye miili ya watoto wao wakati ilipokuwa ikifanyiwa uchunguzi na madaktari.

Maureen ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent aliyetekwa Agosti 21 huku Ikram akitekwa Agosti 25 na Septemba 5 miili yao kukutwa kwenye eneo hilo.

 

Akizungumza na MTANZANIA jana, baba Maureen, David Njau, alisema juzi jioni alikuwa hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, akishuhudia uchunguzi wa mwili wa mwanaye uliofanywa na madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Alisema wakati wa uchunguzi hakuweza kuchunguza sana ila aliona majeraha sehemu za kichwani,sikioni pamoja na kwenye mguu wa mwanaye.

“Siwezi kulizungumzia sana, mimi baada ya kutambua mwili, hayo mengine sikuchunguza sana. Ameumizwa sehemu ya sikioni ilionekana damu imegandia ndani, sehemu ya mguuni ilikuwa na jereha, hatambuliki sana kwani alikuwa ameharibika, hayo mengine sikuyachunguza nilishindwa nikatoka nje,”alisema Njau.

Salim Kassim ambaye ni babu wa Ikram, alisema licha ya mwili wa mtoto kuharibika sana, ulionekana kuwa na viungo vyote na kusema hawakufuatilia matokeo ya uchunguzi zaidi wa madakatari.

“Nilikuwepo wakati wanamfanyia uchunguzi ila sikuuliza wataalamu zaidi walichokigundua kwani tulikuwa tunataka tu mwili tuuzike,”alisema Kassim.

Ikram alizikwa jana majira ya saa 4 asubuhi katika eneo la Makaburi ya Msikiti wa Olasiti baada ya kufanyiwa ibada nyumbani kwao.

Mwili wa Maureen, unatarajia kuzikwa leo katika  makaburi ya JR-Majengo saa 7 mchana, baada ya ibada inayotarajiwa kufanyika nyumbani kwako Olkierian, Kata ya Olasiti.

Kauli za daktari, Polisi

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Dk. Jackline Urio, alisema miili ya watoto hao ilifanyiwa uchunguzi na wataalamu kutoka hospitali ya KCMC, juzi usiku.

 

Dk.Urio alisema wataalamu waliofanya uchunguzi huo  walishirikiana na Polisi na maji ya uchunguzi huo yapo polisi.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema. “Huwezi kupewa majibu wa uchunguzi, tangu lini majibu wanapewa waandishi? Hiyo ni shughuli ya kiupelelezi utapewaje? Hiyo ni kumbukumbu ya kesi, hiyo ndiyo kesi yenyewe utapewaje majibu sasa?” alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles