Na Editha Karlo,Kigoma
MKUU wa Mkoa Wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga amewaomba wazazi na walezi mkoani Kigoma kusomesha watoto wa kike.
Amewataka kuachana na mtazamo kwamba mtoto wa kike hapaswi kupata elimu.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika katika Kijiji Cha Kinyinya wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, alisema wanawake ni wazalishaji wakubwa shambani na katika tasnia ya viwanda hivyo unapomwelimisha mtoto wa kike unakuwa umeelimisha jamii nzima.
Alisema Siku ya Wanawake Duniani hutoa fursa kwa wanawake wenyewa, jamii, vyama vya siasa, Serikali na mashirika ya kiraia kutafakari kwa undani mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake katika kuleta maendeleo yao.
Alisema; “kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema; Tanzania ya Viwanda, Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko Kiuchumi. Hivyo hatuna budi kuwaheshimu na kuwapa elimu ili kuwajengea uwezo wa kuyatekeleza haya,” alisema.
Maganga alisema kupitia mafanikio yanayopatikana katika shughuli za uzalishaji mali hususani kilimo na viwanda, kila mwananchi anatakiwa kuwekeza katika elimu hasa kuwasomesha watoto wa kike.
"Vipaumbele vya mkoa wetu ni kilimo bora na elimu, hivyo katika kuelekea katika nchi ya viwanda, tutafanikiwa endapo malighafi za shambani zitakuwapo kwa wingi huku wanawake wakitumia nafasi hii katika kuboresha bidhaa hizo na kuwapeleka watoto wao shule," alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala aliwaomba wanaume kuacha tabia za kuwanyanyasa wanawake na kuwanyang'anya fedha zinazotokana na nguvu zao.