Na RAMADHAN HASSAN, KONDOA
BAADHI ya wanawake wanaojifungua katika zahanati na vituo vya afya wilayani Kondoa, wamekuwa wakifungashiwa makondo ya nyuma baada ya kujifungua ili wakatupe wenyewe.
Hatua hiyo inatokana na vituo vya afya na zahanati nyingi wilayani humo kutokuwa na mashimo ya kutupa na kuchoma taka.
Hayo yamebainishwa katika utafiti uliofanywa na Shirika lisilo la Serikali la Sikika, kupitia mradi wa ufuatiliaji na uwajibikaji wa jamii katika huduma za afya (SAM) kwenye vituo vya afya na zahanati za Wilaya ya Kondoa.
Mratibu wa Sikika Wilaya ya Kondoa, Omar Said alisema katika utafiti huo waligundua vituo vingi havina mashimo ya kutupia kondo la nyuma kwa wanawake wanaojifungua hatua ambayo huwalazimu wauguzi kuwafungia ili wakatupe majumbani mwao jambo ambalo ni hatari kwa afya.
“Kwa mfano Hospitali ya Wilaya ya Kondoa ambayo ndiyo hospitali kubwa ya wilaya haina eneo la kichomea taka huku zahanati za Bahi na Busi pekee ndiyo zenye mashimo hayo.
“Baadhi ya zahanati zimepokea fedha za Matokeo Makubwa Sasa (BRN) Sh milioni 10 kwa kituo na wameshauri zitumike katika ujenzi wa mashimo ya kutupia kondo la nyuma,” alisema.
Alisema utafiti huo pia ulibaini wauguzi wa zahanati za Baura na Humai katika wilaya hiyo, wamekuwa wakitumia majengo ya wodi za wazazi kama makazi yao baada ya zahanati hizo kukosa nyumba kwa ajili ya wauguzi hao.
Alisema hatua hiyo pia imesababisha msongamano katika wodi ya wazazi.
Utafiti huo pia ulibaini kuwa katika mwaka wa fedha 2014/15 upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya ulikuwa wa kuridhisha lakini kwa mwaka 2016 ulifikia asilimia 86 kutokana na huduma za Bima ya Afya (NHIF) na CHF.
Akizungumzia suala hilo, Mganga wa Wilaya ya Kondoa, Dk. Rashidi Ikaji alisema zimetengwa fedha kwa ajili ya kutengeneza mashimo ya kutupia taka kuondoa tatizo hilo.
“Kondoa kuna changamoto ya vituo vichache vya afya ambako katika vijiji 80 kuna vituo vya afya 24 na kata 21 kuna vituo vinne huku vingi vikiwa havina mashimo kwa ajili ya kutupia makondo hayo.
“Kuhusu watumishi kuishi katika wodi za wazazi, ni kweli katika Zahanati ya Humai yenye vyumba zaidi ya 13 ni vyumba viwili tu ndiyo vinatumika kama makazi ya wauguzi.
“Pia katika Zahanati ya Baura ambayo nayo ina vyumba 13 ni chumba kimoja tu kinachotumika kama makazi, ni changamoto ambazo tunajitahidi kuzitatua,” alisema.