NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAZAZI ambao watoto wao watapotea katika kipindi cha sikukuu watalisaidia Jeshi la Polisi, ikiwamo kutoa maelezo ni kwa nini wamepotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Advera Bulimba, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Tutawaita watusaidie wakati watoto wanapotea wao walikuwa katika mazingira gani, maana imekuwa ni kawaida kipindi cha sikukuu vituo vya polisi vinajaa watoto waliookotwa katika maeneo mbalimbali, ikiwamo fukwe za bahari,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kulewa kupita kiasi, hasa wale wanaoendesha vyombo vya moto na kwamba wakikamatwa sheria itachukua mkondo wake.
“Kwa ujumla wananchi wajue kwamba jeshi lao limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kuelekea msimu huu wa sikukuu.
“Uzoefu unaonyesha sikukuu za mwisho wa mwaka huambatana na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao, utumiaji wa vilevi kupita kiasi, utapeli, wizi, unyang’anyi na uendeshaji wa vyombo vya moto bila kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, askari watafanya doria wakati wote,” alisema.
Aliwataka pia watu wanaomiliki nyumba za kulala wageni na maduka makubwa kama vile hoteli na ‘supermarket’ kufunga kamera za usalama.
“Wafunge kamera ili waweze kufuatilia kila kinachoendelea katika maeneo yao, nani kaingia, nani katoka na anafanya nini,” alisema.
Pia, aliwaonya wafanyabiashara wanaomiliki kumbi za starehe, huku likiwataka kuzingatia masharti ya leseni zao walizopewa hasa msimu huu wa sikukuu.
Amewataka wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie kiwango cha idadi ya watu wanaoruhusiwa kuingia ukumbini na iwapo watagundulika kuzidisha watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Tumegundua katika msimu wa sikukuu kuna baadhi ya watu hupenda kuitumia fursa hiyo kujipatia kipato kisicho halali.
“Tutapita hadi kwenye kumbi za starehe, tukikuta mtu ameruhusu watu zaidi ya kiwango cha leseni yake tutamchukulia hatua za kisheria,” alisema.