27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MVUA YAUA MTOTO, YAEZUA NYUMBA 158

pouring-rain

Na ELIUD NGONDO-SONGWE           

ZAIDI ya nyumba 158 za Kijiji cha Mbebe, mkoani hapa, zimeezuliwa na upepo ulioambatana na mvua ya mawe na kusababisha kifo cha mtoto mmoja (6) baada ya kuangukiwa na ukuta wa moja ya nyumba hizo.

Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana. Mvua hiyo iliyonyesha kwa zaidi ya dakika 30, pia imesababisha nyumba nyingine kubomoka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje, Haji Mnasi, aliwatembelea waathirika hao na kusema kuwa mvua hiyo imeleta janga ambalo wananchi wa kijiji hicho hawakutegemea.

Mnasi alisema kaya 53 hazina makazi kabisa ya kuishi na nyingine zinahitaji marekebisho kidogo huku suala la chakula likiwa si kubwa sana.

“Serikali itahakikisha wananchi wake wanaendelea kuishi kwenye makazi yao pamoja na taasisi zilizoathirika ambazo ni Shule ya Msingi Mbebe ambayo vyumba viwili vya madarasa vimeezuliwa paa zake na saruji mifuko 15 imeharibika.

“Nyingine ni nyumba ya mwalimu wa Shule ya Msingi Mapogolo, ghala la chakula, ofisi ya kata, kituo cha mifugo majengo mawili yameezuliwa mapaa yake, Kanisa la Last Church of God, Kanisa la Moravian na ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbebe, Raison Kashililika, alisema pamoja na kifo cha mtoto huyo, kuna majeruhi 21 ambao wawili kati yao walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje na wengine 19, walitibiwa katika Kituo cha Afya Mbebe.

Kashililika aliwataja waliopata majeraha makubwa ni Betres Mgode na Sabina Sichinga wakazi wa Mbebe, huku mwili wa mtoto Joshua umezikwa katika Kijiji cha Shinji.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Ubatizo Songa, alisema halmashauri itaendelea kufanya jitihada kuhakikisha wananchi wanarejea katika makazi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles