Ashura Kazinja-Morogoro
WATU wawili wamefariki dunia papo hapo kwa kuteketea na moto huku wengine watano wakijeruhiwa, mara baada ya magari kugongana uso kwa uso na kuwaka moto katika eneo la Makungaya, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alisema tukio hilo limetokea jana saa 11 alfajiri.
Magari yaliyohusika ni lori aina ya Scania lenye namba za usajili JA 4417, ambalo lilikuwa limebeba kontena la mkaa na Ashok Leyland lenye namba za usajili T 661 DKS lililokuwa limebeba mtambo wa kuchimbia visima vya maji.
“Magari haya moja lilikuwa likitokea upande wa Mkoa wa Morogoro kuelekea Kagera na jingine lilikuwa likitokea upande wa Dodoma, hata hivyo chanzo cha ajali hii bado hakijajulikana.
“Mpaka sasa tuna vifo vya watu wawili, akiwemo dereva aliyekuwa akiendesha gari la Ashok, dereva wa Scania tumeshindwa kumtambua kwani ameteketea vibaya na moto,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Alisema baada ya kupata taarifa za ajali hiyo, walifanikiwa kufika mapema katika eneo hilo, ili kuweza kusogeza magari yaliyokuwa yameziba barabara na kuzima moto uliowaka, juhudi ambazo zilifanikiwa.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, akiwemo Mateso Khamis walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu ya haraka.
“Ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa gari la Scania lililokuwa limebeba mkaa kushindwa kulimudu wakati akijaribu kumkwepa dereva wa pikipiki, ambaye alikuwa katikati ya barabara na kisha kwenda kugongana uso kwa uso na gari jingine ambalo lilikuwa limebeba mtambo wa kuchimbia visima na kusababisha moto huo kuwaka,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rita Lyamuya, alisema majeruhi wote watano ni wanaume na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
“Ni kweli leo asubuhi tumepokea maiti moja na majeruhi watano huku maiti nyingine tukielezwa imeshindwa kutolewa kutokana na kuteketea kwa moto, majeruhi tuliopokea wote ni wanaume, na walikuwa wameumia maeneo ya vichwani na miguuni, hata hivyo wanaendelea vizuri,” alisema.
Hata hivyo Kamanda Mutafungwa alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijabainika na kwamba uchunguzi unaendelea.