23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Kina Maimu wasomewa mashtaka 100

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ((NIDA), Dickson Maimu na wenzake watano wamefunguliwa upya mashtaka 100 yakiwemo ya kutakatisha fedha 25, kumdanganya mwajiri 43, kughushi 22, kusababisha hasara matano, kujipatia fedha mawili na moja kutumia madaraka vibaya.

Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani aliyekuwa mshtakiwa katika kesi iliyofutwa ameachiwa huru kwani katika hati mpya ya mashtaka hakuwemo.

Washtakiwa waliosomewa mashtaka walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019.

Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Simon Wankyo akisaidiana na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai, aliwataja washtakiwa kuwa ni Maimu, Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Wankyo alidai shtaka la kwanza linamkabili Maimu, Ndege na Ntalima ambao wanadaiwa kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31 mwaka 2015 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa jumla ya Sh 1,175,785,600.93 dhidi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) .

Alidai mshtakiwa Maimu na Sabina wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, Novemba 7 mwaka 2011 maeneo ya Nida kwa matumizi mabaya ya madaraka walisababisha Shule ya Sheria na M-S Law Partner kujipatia faida ya Sh 899,935,494.

Wakili Swai alidai washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka matano ya kuisababishia Nida hasara ya jumla ya Sh 1,690,893,612.91 na mshtakiwa wa tatu, Ndege na mshtakiwa wa tano Silverius wanashtakiwa kwa mashtaka mawili ya kujipatia jumla ya Sh 91,031,922.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha hizo huku wakijua ni mazalia ya kosa la kughushi.

Inadaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama, 43 ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri na mashtaka 22 ya kughushi.

Washtakiwa wanne wanakabiliwa jumla ya mashtaka 25 ya kutakatisha fedha na washtakiwa wawili wamenusurika kuingia katika mashtaka hayo, ambapo wao wanadaiwa kutumia madaraka vibaya kwa mshtakiwa wa sita, Sabina na kusababisha hasara ya Sh 402,210,885.02, shtaka linalomkabili mshtakiwa Mombuli.

Katika shtaka la kutakatisha fedha Maimu anakabiliwa na shtaka moja ambapo anadaiwa kati ya Julai 19 mwaka 2011 na Agosti 31 mwaka 2015, Dar es Salaam, alijiingiza katika muamala wa fedha wa Sh 175,785,600.93 kwa kutoa fedha hizo katika akaunti namba 1408328000  Benki ya CRDB kwa ajili ya Kampuni ya Bima ya Aste wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Swai alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na tayari walishawasilisha taarifa Mahakama Kuu hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi.


Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi kisha kesi ihamie Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Washtakiwa wote wamepelekwa Gereza la Segerea, watarudi mahakamani tarehe iliyopangwa na Mahakama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles