24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania ya pili mapambano dhidi ya rushwa Afrika Mashariki

LONDON, UINGEREZA

RWANDA na Tanzania zimeongoza ukanda wa Afrika Mashariki katika mapambano dhidi ya rushwa huku Kenya ikishuka licha ya juhudi zinazofanywa a Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Shirika la Kimataifa la Transparency International (TI) limetoa ripoti mpya inayoangazia rushwa katika viwango vya kimataifa.

Kwa mujibu wa TI, ukanda wa Afrika Mashariki, Rwanda iliendelea kuongoza kwa kupata alama 56 kati ya 100 na kushika nafasi ya 48 duniani, ikifuatiwa na Tanzania iliyopata alama 36 kati ya 100 na nafasi ya 99 duniani.

Kenya ilifuatia kwa alama 27 kati ya 100 ikiwa imeshuka kutoka alama 28 ilizopata mwaka jana na kushika nafasi ya 144 kati ya mataifa 180 duniani.

Uganda ilipata alama 26 na kushika nafasi ya 149 duniani, Burundi alama 17 nafasi ya 170, Sudan alama 16, nafasi ya 172 na Sudan Kusini alama 12, nafasi ya 178 duniani.

Lakini pia ripoti hiyo imebainisha hali ya kutisha kuhusu vitendo vya rushwa duniani, ikifichua kuwa theluthi moja ya nchi 180 zilipata alama chini ya 50 kati ya 100 wakati alama za wastani kwenye nchi zote zikiwa ni ndogo – alama 43.

Kwenye faharasa yake kuhusu ufisadi ambayo imechapishwa jana, taasisi hiyo isiyo ya kiserikali imesema kushindwa kwa jumla   kudhibiti rushwa kunachangia mgogoro wa demokrasia duniani kote.

Kwa kuzingatia maeneo ya  kanda nchi za Ulaya ya Magharibi na hasa za Umoja wa Ulaya, ndizo zimepata wastani wa alama 66.  Na zilizoshika mkia ni zile za Afrika   Kusini mwa Jangwa la Sahara, zikiwa na  wastani wa alama 33.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bara la Afrika limeshindwa kutafsiri ahadi zake za kupambana na rushwa katika maendeleo halisi.

Nchi ambazo zinakabiliwa na vita zikiwamo Somalia, Syria na Sudan Kusini zina viwango vya juu vya ufisadi.

Mwanaharakati wa kupambana na ufisadi  Kenya, Okiya Omutata, amesema vita dhidi ya rushwa vinaendeshwa kwa maneno tu bila matendo licha ya  kuwa haviendeshwi kwa uwazi na ukweli. ”Siasa nyingi ndizo zinapigwa.

“Hatuoni kazi ikifanyika kama inavyostahili. Ukiangalia mashtaka kortini, pia hayana uzito, ushahidi haupo, na ukiangalia wanajaribu tu kuonyesha kuwa wanafanya kazi, lakini si kwamba wanataka kuung’oa ufisadi na mzizi wake ili utupwe mbali,” alisema.

Denmark na New Zealand zimeendelea kuongoza kuwa nchi zenye vitendo vichache vya rushwa katika miaka ya hivi karibuni na ziliongoza pia mwaka uliopita wa 2018.

Denmark ilipata alama 88, na New Zealand ya pili kwa kuwa na alama 87. Finland, Singapore, Sweden, Uswisi, Norway, Uholanzi, Canada, Luxembourg, Ujerumani na Uingereza zinashikilia nafasi 10 za juu.

Ni mara ya kwanza kwa Marekani kutoingia kwenye nchi 20 zisizokuwa na hali mbaya ya  ufisadi tangu mwaka 2011.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles