Na PENDO FUNDISHA -MBEYA
SIKU moja kabla ya mtihani wa taifa wa darasa la saba kuanza, ofisi ya Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Meta ya jijini hapa imevunjwa na watu wasiojulikana, wakidhani kwamba mitihani hiyo imehifadhiwa huko.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema siku moja kabla ya mitihani ya darasa la saba kufanyika siku ya Jumatano, watu hao wasiojulikana walivamia ofisi hiyo usiku na kuivunja.
Alisema watu hao waliingia ndani ya ofisi hiyo na kujaribu kuvunja chumba maalumu cha kuhifadhia nyaraka muhimu (strong room) ikiwemo mitihani ya taifa.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba watu hao walipoingia ndani ya ofisi walipekua vitu mbalimbali na baadae kuvunja kasiki ya kuhifadhia nyaraka mbalimbali muhimu, lakini hawakuweza kuondoka na kitu chochote.
“Lakini uchunguzi unaendelea kuwabaini wahalifu hao ambao lengo lao huenda lilikuwa kuiba mitihani ambayo nayo haikuhifadhiwa shuleni hapo,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, James Kasusura, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kwamba watu hao walikuwa na nia ya kuiba mitihani ya taifa ya darasa la saba.
“Serikali ilibadilisha mfumo wa uhifadhi wa mitihani ya taifa, awali ilikuwa ikihifadhiwa kwenye shule, lakini sasa inahifadhiwa sehemu moja tu, katika ofisi maalumu ya wilaya, hivyo njama zao ziligonga mwamba,” alisema.
Wanafunzi 960,202 nchini wamefanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wakiwamo wasichana 503,972 sawa na asilimia 52.49 na wavulana 456,230 sawa na asilimia 47.51.