SERIKALI imewasimamisha kazi watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa muda usiojulikana kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 70.
Vilevile imemfukuza kazi mhasibu mmoja wa Hospitali Teule ya Machame kwa tuhuma hizo hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Antony Mtaka, alisema jana kuwa watumishi hao wamesimamishwa kazi baada ya kuthibitika kufanya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.
Alisema wawili kati yao ni maofisa wa halmashauri hiyo ambao wanadaiwa kuhusika na upotevu wa zaidi ya Sh milioni 38.
“Fedha hizo zilikuwa za malipo ya muda wa ziada wa saa za kazi za watumishi wa Hospitali Teule ya Machame,” alisema.
Mtaka aliwataja watumishi hao kuwa ni Valentine Gisha na Edewin Kalokola, ambao wanadaiwa kushirikiana na Mhasibu wa Hosptali hiyo, Philipo Massasi.
Alisema Serikali pia imewasimamisha maofisa wawili wa idara ya utumishi wa Halmashauri ya Hai wanadaiwa kughushi nyaraka za madaktari waliokwisha kuacha kazi.
Mtaka alidai watumishi hao walitumia nyaraka na majina ya watumishi hao kuchukua mikopo wa zaidi ya Sh milioni 36 kutoka benki ya CRDB.
Aliwataja watumishi waliohusika na kughushi huko kuwa ni Faraja Nandatu na Isaya Buhege.
Alisema watumishi hao wamekwisha kupewa barua za kusimamishwa kazi na vyombo vinavyohusika ikiwamo TAKUKURU vinaendelea na uchunguzi.
Mtaka alizitaka taasisi za fedha kujitathimi kuhusiana na watumishi wake ambao baadhi hushirikiana na watumishi wa serikali kufanya utapeli.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Fredy Kweka, alisema watumishi hao wane walisimamishwa kazi tangu Novemba 11.