29.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kufutwa uchaguzi Z’bar kaa la moto

awadhNa Mwandishi Wetu, Zanzibar

UAMUZI wa Serikali wa kutoa tamko la kufutwa kwa Uchaguzi wa Zanzibar umezua maswali kwa wananchi, huku Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (Zanzibar Law Society), Awadh Ali Said, akisema suala hilo ni la aibu kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amesema hatua ya kushindwa kuainisha vifungu vya Katiba ya Zanzibar kuhusu kufutwa kwa matokeo kwa tamko la mwenyekiti kwa kutaja vifungu vya kisheria visivyohusika ni wazi Serikali imeshikwa pabaya.

Awadh aliyasema hayo jana kupitia taarifa yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na kueleza kuwa amepitia tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ambalo linaeleza kuwa tume imefuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema katika tamko hilo, Jecha ametaja kifungu kimoja cha Katiba ya Zanzibar (kif 119 (10) ) na vifungu viwili vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar No 11ya 1984 ( kif 3(1) na 5(a.)

“Naomba tuvidurusu hivi vifungu tuone je, vinatoa mamlaka ya ufutaji uchaguzi/matokeo au vinahusu mambo mengine? Katiba kifungu 119(10); Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamo Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa tume ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi.

“Sheria ya Uchaguzi No 11 ya 1984, Kifungu 3(1) Kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo Tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa, itajaaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria kama yametiwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi.

“…Kifungu  5 (a): Tume itakuwa na majukumu ya; a)Usimamizi mzima wa mienendo ya jumla katika uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, na viongozi wa Serikali za mitaa kwa Zanzibar,” alisema Awadh.

Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, alisema kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar kinaelezea akidi  ya kikao cha tume, ambapo alihoji kilivyohusishwa kwa makosa.

“Hapo kinahusikaje na uwezo wa kufuta uchaguzi na matokeo yake? Kifungu cha 3(1) cha sheria ya uchaguzi, kinazungumzia kuwa uchapishaji wa kanuni, maelekezo na taarifa za tume zitatolewa kwa saini ya mwenyekiti au mkurugenzi je, kinahusikanaje na uwezo wa kufuta uchaguzi wa matokeo hapo?

“Kifungu cha 5(a) cha sheria kinazungumzia jukumu la tume, kuwa msimamizi wa jumla wa uchaguzi unaofanywa Zanzibar. Kinahusiana vipi na uwezo wa kufuta uchaguzi na matokeo yake? Aibu kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu,” alisema Awadh

“Ama kweli mfa maji hukamata maji,” aliongeza.

Juzi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ilitoa tamko la kisheria la kufuta uchaguzi wa Zanzibar.

Katika kumaliza mgogoro huo uliovikumba visiwa vya Zanzibar, hivi sasa zimekuwa zikifanyika juhudi mbalimbali ikiwamo mazungumzo kwa kuwashirikisha waliokuwa marais wastaafu wa Zanzibar.

Pamoja na hali hiyo, pia juzi Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth) zimemteua Rais mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan na kumpa  jukumu jipya la kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huo wa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo, Jonathan aliongoza Jopo la Uangalizi la Jumuiya ya Madola (COG) katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.

Jumuiya ya Madola inaundwa na nchi 53 zilizowahi kutawaliwa na Uingereza ikiwamo Tanzania.

Taarifa ya jumuiya hiyo ilieleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, ulishuhudia Dk. John Magufuli akiwa Rais wa Tanzania wa awamu ya tano, huku timu hiyo ya uangalizi ikiridhia uchaguzi huo wa Jamhuri ya Muungano, kwamba ni halali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles