Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SERIKALI imetangaza kuwapandisha vyeo watumishi wa umma 193,166 kuanzia Mei Mosi.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wakati akitoa kauli kuhusu upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma.
Mkuchika alipewa nafasi hiyo na Spika wa Bunge, Job Ndugai mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
Alisema watumishi hao watakaopandishwa vyeo ni wenye utendaji kazi mzuri ambao wanakaribia kustaafu, watumishi waliokaa katika vyeo walivyonavyo kwa muda usiopungua miaka minne na kukasimiwa kwenye ikama ya bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.
Mkuchika aliwataka waajiri wote kuhakikisha wanawapandisha vyeo watumishi stahiki kwa wakati na kwa kuzingatia TANGE (Seniority List) ya taasisi husika, sifa za kimuundo na kuwepo kwa nafasi iliyoidhinishwa kwa mujibu wa matokeo ya tathimini ya utendajikazi.
“Waajiri na maofisa watakaotekeleza zoezi hili kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu upandishaji vyeo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma,” alisema.
Alisema upandishwaji vyeo ulihairishwa Mei mwaka 2016 kupisha uhakiki wa watumishi hewa na mishahara batili pamoja na vyeti vya utumishi wa umma.
“Baada ya kukamilika kwa mazoezi tajwa, Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli aliridhia upandishaji vyeo watumishi kwa awamu,” alisema.
Mkuchika alisema awamu ya kwanza iliyoanza Novemba Mosi mwaka juzi, ilihusisha upandishaji na uidhinishaji wa taarifa za watumishi 59,967 ambao taarifa zao za kupandishwa vyeo zilikuwemo katika Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS), lakini zilikuwa hazijaidhinishwa wakati wa usitishaji tajwa Mei mwaka 2016.
Alisema kuwa awamu ya pili iliyoanza Aprili Mosi mwaka jana, ilihusisha watumishi zaidi ya 53,553 ambao walipandishwa vyeo, lakini taarifa zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye mfumo wa HCMIS.
Mkuchika alisema uidhinishaji wa taarifa za watumishi 113,520 katika makundi hayo mawili kupitia mfumo wa HCMIS umekamilika. “Baada ya kukamilika upandishaji vyeo watumishi wa umma wapatao 113,520, Serikali imewaelekeza waajiri kuendelea na upandishaji vyeo kwa watumishi 193,116 waliokasimiwa ikama na bajeti ya mishahara kwa mwaka wa fedha 2017/18 kuanzia Mei mwaka huu,” alisema Mkuchika